The chat will start when you send the first message.
1Akaingia Kapernaumu tena, baada ya siku kadhaa, ikasikiwa ya kwamba yumo nyumbani.[#Mt 9:1-8; Lk 5:17-26]
2Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake.
3Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne.
4Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kulivunja wakaliteremsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza.
5Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.
6Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao,
7Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?[#Isa 43:25]
8Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu?
9Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?
10Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza),
11Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.
12Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Hatujawahi kuona jambo kama hili kamwe.
13Akatoka tena, akaenda kando ya bahari, mkutano wote ukamwendea, akawafundisha.[#Mt 9:9-13; Lk 5:27-32]
14Na alipokuwa akipita, akamwona Lawi wa Alfayo, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaondoka akamfuata.[#Yn 1:43]
15Na alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi na wenye dhambi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwa maana walikuwa wengi wakimfuata.
16Na Waandishi na Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?
17Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.
18Nao wanafunzi wake Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwa nini wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?[#Mt 9:14-17; Lk 5:33-38]
19Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana arusi pamoja nao hawawezi kufunga.
20Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku ile.
21Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; akishona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi.
22Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya.
23Ikawa alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke.[#Mt 12:1-8; Lk 6:1-5; #Kum 23:25]
24Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato?
25Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa akiona njaa na kuhitaji chakula, yeye na wenziwe?[#1 Sam 21:1-6]
26Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alipokuwa kuhani mkuu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kuliwa ila na makuhani, akawapa na wenziwe?[#Law 24:9]
27Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato.[#Kum 5:14]
28Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.