Nehemia 3

Nehemia 3

Utaratibu wa kazi

1Ndipo akaondoka Eliashibu, kuhani mkuu, pamoja na nduguze makuhani, wakalijenga lango la kondoo; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake; mpaka mnara wa Hamea wakalitakasa, mpaka mnara wa Hananeli.[#Neh 12:10,39; Yn 5:2; Yer 31:38; Zek 14:10]

2Sehemu iliyofuata ilijengwa na watu wa Yeriko. Na baada yao Zakuri mwana wa Imri akajenga.[#Ezr 2:34; Neh 7:36]

3Na lango la samaki wakalijenga wana wa Senaa; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake.[#2 Nya 33:14; Neh 12:39; Sef 1:10; Neh 6:1]

4Na baada yao akaijenga Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi. Na baada yao akafanyiza Meshulamu, mwana wa Berekia, mwana wa Meshezabeli. Na baada yao akafanyiza Sadoki, mwana wa Baana.

5Na baada yao wakajenga Watekoi; lakini wakuu wao hawakutia shingo zao kazini mwa bwana wao.[#Amu 5:23]

6Na lango la kale wakalijenga Yoyada, mwana wa Pasea, na Meshulamu, mwana wa Besodeya; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake.[#Neh 12:39]

7Na baada yao wakajenga Melatia, Mgibeoni, na Yadoni, Mmeronothi, watu wa Gibeoni, na wa Mispa, waliokuwa chini ya utawala wa mtawala wa sehemu ya ng'ambo ya Mto.[#Yos 9:3; Neh 2:8]

8Na baada yao akajenga Uzieli, mwana wa Harhaya, mmoja wa mafundi wa dhahabu. Na baada yake akafanyiza Hanania, mmoja wa mafundi wa manukato, nao wakaujengea Yerusalemu buruji mpaka ule ukuta mpana.[#Neh 12:38]

9Na baada yao Refaya, mwana wa Huri akajenga, mtawala wa nusu ya Yerusalemu.[#3:9 Au msimamizi wa sehemu aliyokabidhiwa.]

10Na baada yao akajenga Yedaya, mwana wa Harumafu, kuielekea nyumba yake. Na baada yake akajenga Hatushi, mwana wa Hashabneya.

11Malkiya, mwana wa Harimu, na Hashubu, mwana wa Pahath-moabu, wakajenga sehemu nyingine, na mnara wa tanuri.[#Ezr 2:32]

12Na baada yake akajenga Shalumu, mwana wa Haloheshi, mtawala wa nusu ya sehemu ya Yerusalemu, yeye na binti zake.[#Kut 35:25; Lk 8:3; Flp 4:3; #3:12 Tazama 3:9.]

13Lango la bondeni wakalijenga Hanuni, nao wakaao Zanoa; wakalijenga, wakaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake, na huo ukuta wa dhiraa elfu moja mpaka lango la jaa.[#Neh 2:13; Yos 15:34]

14Na lango la jaa akalijenga Malkiya, mwana wa Rekabu, mtawala wa sehemu ya wa Beth-hakeremu; akalijenga, akaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake.[#Yer 6:1; Mik 1:11]

15Na lango la chemchemi akalijenga Shalumu, mwana wa Kolhoze, mkuu wa Mispa akalitengeneza lango la Chemchemi akalijenga na kulifunika, akasimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake, na huo ukuu wa birika la Shiloa karibu na bustani ya mfalme, mpaka madaraja yashukayo kutoka mji wa Daudi.[#Neh 2:14; Yos 18:26; Amu 20:1-3; Yer 40:6; Isa 8:6; Lk 13:4; Yn 9:7]

16Baada yake akajenga Nehemia, mwana wa Azbuki, mkuu wa nusu ya mtaa wa Beth-suri, mpaka mahali paelekeapo makaburi ya Daudi, na mpaka birika lililofanyizwa, na mpaka nyumba ya wapiganaji.[#2 Fal 20:20; Isa 22:11; Wim 3:7]

17Baada yake wakajenga Walawi, Rehumu, mwana wa Bani. Baada yake akajenga Hashabia, mkuu wa nusu ya mtaa wa Keila, kwa mtaa wake.

18Baada yake wakajenga ndugu zao, Binui, mwana wa Henadadi, mkuu wa nusu ya mtaa wa Keila.[#Yos 15:44; 1 Sam 23:1]

19Na baada yake Ezeri, mwana wa Yeshua, mkuu wa Mispa, akajenga sehemu nyingine, inayoelekeana na njia ya kupanda kwa ghala ya silaha, pembeni mwa ukuta.[#2 Nya 26:9]

20Baada yake Baruku, mwana wa Zakai, akajenga kwa bidii sehemu nyingine, kutoka pembeni mwa ukuta mpaka mlango wa nyumba ya Eliashibu, kuhani mkuu.[#Mhu 9:10; Rum 12:11]

21Baada yake akajenga Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, sehemu nyingine, kutoka mlangoni mwa nyumba ya Eliashibu mpaka mwisho wa nyumba ya Eliashibu.

22Na baada yake wakafanyiza makuhani, watu wa Uwandani.

23Baada yao wakajenga Benyamini na Hashubu, kuielekea nyumba yao. Baada yao akajenga Azaria, mwana wa Maaseya, mwana wa Anania, kando ya nyumba yake.

24Baada yake Binui, mwana wa Henadadi, alitengeneza sehemu nyingine, kuanzia kwenye nyumba ya Azaria mpaka ugeukapo ukuu, na mpaka pembeni.

25Baada yake akajenga Palali, mwana wa Uzai, kuelekea ugeukapo ukuta, nao mnara utokezao penye nyumba ya juu ya kifalme, iliyopo karibu na uwanda wa walinzi. Baada yake akajenga Pedaya, mwana wa Paroshi,[#Neh 12:39; Yer 32:2]

26(basi Wanethini hukaa Ofeli), mpaka mahali paelekeapo lango la maji kukabili mashariki, nao mnara utokezao.[#Ezr 2:43; Neh 7:46; 8:1-3]

27Baada yake wakajenga Watekoi sehemu nyingine, kuuelekea mnara mkubwa utokezao, na mpaka ukuta wa Ofeli.

28Juu ya lango la farasi wakajenga makuhani, kila mtu kuielekea nyumba yake. Baada yao akajenga Sadoki, mwana wa Imeri, kuielekea nyumba yake.[#2 Fal 11:16; 2 Nya 23:15; Yer 31:40]

29Na baada yake akajenga Shemaya, mwana wa Shekania, mlinzi wa lango la mashariki.[#Yer 19:2]

30Baada yake wakajenga Hanania, mwana wa Shelemia, na Hanuni, mwana wa sita wa Salafu, sehemu nyingine. Baada yake akafanyiza Meshulamu, mwana wa Berekia, sehemu nyingine kuelekea chumba chake.

31Baada yake akajenga Malkiya, mmoja wa mafundi wa dhahabu, mpaka nyumba ya Wanethini, na ya wafanya biashara, kulielekea lango la gereza, na mpaka chumba cha juu cha pembeni.

32Na kati ya chumba cha juu cha pembeni na lango la kondoo wakajenga mafundi wa dhahabu na wafanya biashara.[#Neh 12:39; Yn 5:2]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya