The chat will start when you send the first message.
1Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakubakia mapengo ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango);[#Neh 2:10; 3:1-3]
2Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Lakini wakakusudia kunifanyia mabaya.[#Mit 26:24; 1 Nya 8:12; Neh 11:25,35; Zab 12:2; Mit 26:24; Mhu 4:4; Mik 7:4,5]
3Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, siwezi kushuka, kwa nini niwashukie na hapo kazi isimame?[#Mit 14:15]
4Nao wakaniletea mwito huo mara nne; nikawajibu maneno yale yale.[#Mit 1:10]
5Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumishi wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake;
6nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mnakusudia kuasi; ndiyo sababu unaujenga huo ukuta; nawe unataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo.[#Yer 9:3; Rum 3:8; 2 Kor 6:8; 1 Pet 2:12; Neh 2:19; Ezr 4:13; Lk 23:2]
7Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu kwa kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa mfalme ataarifiwa mambo haya, Basi sasa, njoo ili tushauriane.
8Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni.[#Ayu 13:4; Zab 36:3; Isa 59:4; Dan 11:27]
9Kwani hao wote walitaka kutuogofya, wakisema, Kwa kuwa mikono yao italegea katika kazi, kazi isifanyike. Lakini sasa Ee Mungu, itie nguvu mikono yangu.[#Kum 33:25; Zab 56:3; Isa 41:10; 2 Kor 12:9]
10Nikaingia nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa kifungo cha nyumbani; naye akasema, Tukutane nyumbani mwa Mungu, ndani ya hekalu, na tuifunge milango ya hekalu; kwa kuwa watakuja kukuua; naam, wakati wa usiku watakuja kukuua.[#Mit 26:24]
11Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia.[#Mit 28:1]
12Nikatambua, na tazama, si Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; kwa kuwa Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.[#Eze 13:22]
13Kwa sababu hii aliajiriwa, ili mimi niogope, nikafanye hivyo na kutenda dhambi, kisha wao wawe nazo habari mbaya, ili wanishutumie.
14Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, Tobia na Sanbalati kulingana na hayo matendo yao, na yule nabii mwanamke Noadia.[#Neh 13:29; Eze 13:17; #6:14 Noadia maana yake yule ambaye BWANA hukutana naye (Ezr 8:33), na hao manabii waliosalia, waliotaka kuniogofya.]
15Basi huo ukuta ukakamilika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli, katika muda wa siku hamsini na mbili.
16Ikawa adui zetu wote waliposikia, ndipo wamataifa wote waliotuzunguka wakaogopa, nao wakakata tamaa sana machoni pao wenyewe; maana waliitambua kazi hiyo ilivyotendwa na Mungu wetu.[#Neh 2:10; 4:1; 6:1; Zab 126:2]
17Tena siku zile wakuu wa Yuda walimtumia nyaraka nyingi Tobia nazo nyaraka za Tobia ziliwafikia.
18Kwa maana walikuwa watu wengi katika Yuda waliomwapia, kwa sababu alikuwa mkwewe Shekania, mwana wa Ara; naye Yehohanani mwanawe amemwoa binti Meshulamu, mwana wa Berekia.
19Tena waliyanena mema yake mbele yangu, na kumwambia maneno yangu. Tobia naye akaniletea mimi nyaraka za kuniogofya.