The chat will start when you send the first message.
1Kisha wana wa Israeli, mkutano wote, wakaingia jangwa la Sinai, katika mwezi wa kwanza, watu wakakaa Kadeshi; Miriamu akafa huko, akazikwa huko.[#Hes 33:36; 26:59; Kut 15:20]
2Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakakusanyika Juu ya Musa na juu ya Haruni.[#Kut 17:1-7; 16:2,7-12; Hes 16:19,42; 21:5; 1 Kor 10:10]
3Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingekuwa heri kama tungekufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za BWANA![#Hes 14:2; Kut 17:2; Hes 11:1,33; 14:37; 16:32,33,49; Omb 4:9]
4Mbona mmewaleta kusanyiko la BWANA hadi jangwani hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu?[#Kut 5:21; 17:3; Hes 11:5; Zab 106:21; Mdo 7:35,40]
5Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa.
6Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hadi mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa BWANA ukawatokea.[#Hes 14:5]
7BWANA akasema na Musa, akinena,
8Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao.[#Kut 17:5; Neh 9:15; Zab 78:15,16; Isa 43:20]
9Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za BWANA kama alivyomwamuru.[#Hes 17:10]
10Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu?[#Zab 106:33]
11Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia.[#Yak 1:20; Kut 17:6; Kum 8:15; 1 Kor 10:4]
12BWANA akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa.[#Hes 27:14; Kum 3:26; Law 10:3; Eze 20:41; 36:23; 1 Pet 3:15]
13Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na BWANA, naye alijionesha kuwa mtakatifu kati yao.[#Zab 95:8; #20:13 Maana yake ni ‘gombana’ au ‘nung'unika’.]
14Kisha Musa akatuma wajumbe kutoka Kadeshi wamwendee mfalme wa Edomu, na kusema, Ndugu yako Israeli asema, Wewe wazijua taabu zote zilizotupata;[#Amu 11:16,17; Kum 23:7; Oba 1:10,12]
15jinsi baba zetu walivyoteremkia Misri, nasi tulikaa Misri muda mrefu, nao Wamisri walitutenda vibaya sana, na baba zetu pia;
16tena tulipomlilia BWANA, akatusikiza sauti yetu, akamtuma malaika, na kututoa Misri; nasi tupo hapa Kadeshi, mji wa mpakani mwa nchi yako;[#Kut 2:23; 3:7; Mdo 7:35]
17tafadhali utupe ruhusa tupite katika nchi yako; hatutapita katika mashamba, wala katika mashamba ya mizabibu, wala hatutakunywa maji ya visimani; tutaifuata njia kuu ya mfalme, tusigeuke kwenda upande wa kulia, wala upande wa kushoto, hadi tutakapotoka katika nchi yako.[#Hes 21:22]
18Edomu akamwambia, Hutapita katika nchi yangu, nisije nikakutokea kupigana nawe kwa upanga.
19Wana wa Israeli wakamwambia, Tutakwea kwa njia kuu; tena kama tukinywa maji yako, mimi na wanyama wangu wa mifugo, ndipo nitakulipa thamani yake; nipe ruhusa nipite kwa miguu yangu wala sitaki neno lingine lolote.[#Kum 2:6,28]
20Akamwambia, Hutapita katika nchi yangu. Kisha Edomu akamtokea ili kupigana naye, na watu wengi, na kwa mkono wa nguvu.[#Mwa 27:41; 32:6; Amu 11:17; Zab 120:7; Eze 35:5,11; Amo 1:11]
21Basi hivyo Edomu akakataa kumpa Israeli ruhusa kupita katika mipaka yake; kwa hiyo Israeli akageuka na kumwacha.[#Kum 2:27,29; Amu 11:18; Rum 12:18; Ebr 12:14]
22Kisha wakasafiri kutoka Kadeshi; wana wa Israeli, mkutano mzima, wakafikia mlima wa Hori.[#Hes 33:37; 21:4]
23BWANA akanena na Musa na Haruni katika mlima wa Hori, karibu na mpaka wa nchi ya Edomu, akawaambia,
24Haruni atakusanywa awe pamoja na watu wake; kwa kuwa hataingia katika nchi niliyowapa wana wa Israeli, kwa sababu mliasi kinyume cha neno langu hapo penye maji ya Meriba.[#Mwa 25:8; Hes 27:13; Isa 57:1,2; Ebr 12:23]
25Uwatwae Haruni na mwanawe Eleazari uwalete juu ya mlima wa Hori;[#Kum 32:50]
26umvue Haruni mavazi yake, ukamvike Eleazari mwanawe mavazi hayo; kisha Haruni atakusanywa kwa watu wake, naye atakufa huko.
27Musa akafanya kama BWANA alivyomwagiza; wakakwea katika mlima wa Hori mbele ya macho ya mkutano wote.
28Kisha Musa akamvua Haruni mavazi yake, akamvika mwanawe Eleazari mavazi hayo; Haruni akafa huko katika kilele cha mlima; Musa na Eleazari wakateremka mlimani.[#Kut 29:29; Hes 33:38; Kum 10:6; Hes 23:10; Ayu 30:23; Mit 14:32; Hos 13:14; Ufu 14:13]
29Na mkutano wote ulipoona ya kuwa Haruni amekufa, wakamwombolezea Haruni muda wa siku thelathini, maana, nyumba yote ya Israeli ikamwombolezea.[#Mwa 50:3,10; Kum 34:8]