Hesabu 35

Hesabu 35

Miji kwa makuhani

1Kisha BWANA akanena na Musa katika nchi tambarare za Moabu, karibu na mto wa Yordani, hapo Yeriko, akamwambia,[#Yos 21:1-42]

2Uwaagize wana wa Israeli wawape Walawi miji wapate mahali pa kukaa, katika milki yao; pamoja na malisho yaliyoizunguka hiyo miji kotekote mtawapa Walawi.[#Law 25:32,33; Hes 18:20-24; Kum 18:1,2; 1 Nya 6:64; Yos 14:3,4; 21:2; Eze 45:1; 48:8]

3Hiyo miji watakuwa nayo ili wakae humo, na malisho watakuwa nayo kwa wanyama wao wa mifugo, na kwa mali zao, na kwa wanyama wao wote.

4Na yale malisho ya miji mtakayowapa Walawi, ukubwa wake utakuwa tangu ukuta wa mji kupima kiasi cha dhiraa elfu pande zote.

5Nanyi mtapima hapo nje ya mji upande wa mashariki dhiraa elfu mbili, na upande wa kusini dhiraa elfu mbili, na upande wa magharibi dhiraa elfu mbili, na upande wa kaskazini dhiraa elfu mbili, huo mji ulio katikati. Hayo ndiyo yatakayokuwa kwao malisho ya miji.

6Na hiyo miji mtakayowapa Walawi, itakuwa miji sita ya kukimbilia, mtakayoweka kwa ajili ya mwenye kumwua mtu, ili akimbilie huko; pamoja na hiyo mtawapa miji arubaini na miwili zaidi.[#Kum 4:41; Yos 20:2; 21:3; Zab 9:9; 62:7,8; Isa 4:6]

7Miji yote mtakayowapa hao Walawi jumla yake itakuwa miji arubaini na minane; mtawapa miji hiyo pamoja na malisho yake.[#1 Nya 6:54-81; Yos 21:41]

8Tena katika miji mtakayotoa ya hiyo milki ya wana wa Israeli, katika hao walio wengi mtatwaa miji mingi; na katika hao walio wachache mtatwaa miji michache; kila mtu kama ulivyo urithi wake atakaourithi, atawapa Walawi katika miji yake.[#Yos 21:3; Kut 16:18; Hes 26:54; 33:54]

Miji ya makimbilio

9Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,[#Kum 19:2-4; Yos 20:1-9]

10Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani,[#Kum 19:2; Yos 20:2]

11Ndipo mtajiwekea miji itakayokuwa ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.[#Kut 21:13]

12Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kulipiza kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe.[#Kum 19:6; Yos 20:3]

13Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya kukimbilia.

14Mtawapa miji mitatu ng'ambo ya pili ya Yordani, na miji mitatu mtawapa katika nchi ya Kanaani; miji hiyo itakuwa ni miji ya makimbilio.[#Kum 4:41; 2 Kor 8:13,14]

15Miji hiyo sita itakuwa pa kukimbilia usalama kwa ajili ya wana wa Israeli, kwa ajili ya mgeni na kwa ajili ya aishiye nao kama mgeni; ili kila amwuaye mtu, bila kukusudia kuua, apate mahali pa kukimbilia.[#Hes 15:16]

Kuhusu kuua na kulipiza kisasi cha damu

16Lakini kama alimpiga kwa chombo cha chuma, akafa, ni mwuaji huyo; mwuaji hakika yake atauawa.[#Kut 21:12,14; Law 24:17; Kum 19:11,12]

17Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa.

18Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa.

19Mwenye kutwaa kisasi cha damu ndiye atakayemwua mwuaji; hapo atakapokutana naye, atamwua.

20Tena kama alimsukuma kwa kumchukia au kama alimtupia kitu kwa kumvizia, hadi akafa;[#Mwa 4:8; 2 Sam 3:27; 20:10; 1 Fal 2:31; Lk 4:29; Kut 21:14; Kum 19:11; 1 Sam 18:10,11,25; 20:1; 23:7,8; Zab 10:7-10; 30:7,8]

21au akampiga kwa mkono wake kwa kuwa ni adui, naye akafa; yeye aliyempiga lazima atauawa; yeye ni mwuaji; mwenye kutwaa kisasi cha damu atamwua mwuaji, hapo atakapokutana naye.

22Lakini ikiwa alimsukuma ghafla pasipo kumchukia; au akamtupia kitu chochote pasipo kumvizia,

23au kwa jiwe liwalo lote, ambalo kwa kupigwa kwalo humkini mtu kufa, bila kumwona akamtupia hata akafa, naye hakuwa adui yake, wala hakumtakia madhara;[#35:23 au ‘bila, kukusudia’.]

24ndipo mkutano utaamua kati ya huyo aliyempiga mtu na huyo atakayelipiza kisasi cha damu, kama hukumu hizi zilivyo;[#Yos 20:6]

25nao mkutano utamwokoa yule aliyemwua mtu na mkono wa mwenye kulipiza kisasi cha damu; tena mkutano utamrejesha katika mji wake wa makimbilio, aliokuwa anaukimbilia; naye atakaa humo hata kifo chake kuhani mkuu, aliyepakwa mafuta matakatifu.[#Efe 1:7; Kut 29:7; Law 4:3; 21:10]

26Lakini kama mwenye kumwua mtu akienda wakati wowote kupita mpaka wa huo mji wa makimbilio, alioukimbilia;

27na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwona, naye yuko nje ya mpaka wa mji wake wa makimbilio, na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwua huyo mwuaji, hatakuwa na hatia ya damu;[#Kut 22:2]

28kwa sababu ilimpasa kukaa ndani ya mji wake wa makimbilio hadi kifo chake kuhani mkuu lakini kuhani mkuu atakapokwisha kufa huyo mwuaji atarudi aende nchi ya urithi wake.

29Mambo haya yatakuwa ni amri ya hukumu kwenu, katika vizazi vyenu vyote, katika makazi yenu yote.[#Hes 27:11]

30Mtu yeyote atakayemwua mtu, huyo mwuaji atauawa kwa vinywa vya mashahidi; lakini shahidi mmoja hatashuhudia juu ya mtu akauliwa.[#Kum 17:6; 19:15; Mt 18:16; 2 Kor 13:1; 1 Tim 5:19; Ebr 10:28; Ufu 11:3]

31Tena, msipokee fidia kwa ajili ya uhai wa mwuaji, ambaye amekuwa na hatia ya mauti; Lakini lazima atauawa.

32Tena hamtapokea fidia kwa ajili ya huyo aliyeukimbilia mji wake wa makimbilio, apate kwenda tena kukaa katika nchi, hata kifo cha kuhani mkuu.[#Mdo 4:12; Gal 2:21]

33Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga.[#Mwa 4:9-12; Law 18:25; Kum 21:23; Zab 106:38; Isa 26:21; Hos 4:2,3; Mik 4:11; Mwa 9:6]

34Kwa hiyo msiitie unajisi nchi mwishiyo ambayo nami nakaa kati yake; kwa kuwa mimi BWANA nakaa kati ya wana wa Israeli.[#Law 18:25; Kum 21:23; Kut 29:45,46; Hes 5:3; Zab 76:2; Isa 8:18; Hos 9:3; 2 Kor 6:16]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya