The chat will start when you send the first message.
1Maono yake Obadia.[#Isa 21:11; Eze 25:12-14; Yoe 3:19; Mal 1:3]
Ndivyo asemavyo Bwana MUNGU juu ya Edomu;
Tumepata habari kwa BWANA,
Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa,
Akisema, Haya, inukeni ninyi;
Na tuinuke tupigane naye.
2Tazama, nimekufanya mdogo kati ya mataifa;
Umedharauliwa sana.
3Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,[#2 Fal 14:7; 2 Nya 25:12; Isa 14:13; Ufu 18:7]
Wewe ukaaye katika pango za majabali,
Mwenye makao yako juu sana;
Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi?
4Ujapopanda juu kama tai,[#Ayu 20:6; Isa 14:14,15; Yer 49:16; Amo 9:2; Hab 2:9]
Ijapokuwa kiota chako kimewekwa kati ya nyota,
Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA.
5Kama wezi wangekujia, kama wanyang'anyi wangekujia usiku, (jinsi ulivyokatiliwa mbali!) Je! Wasingeiba kiasi cha kuwatosha? Kama wachumao zabibu wangekujia, je! Wasingeacha baadhi ya zabibu, ziokotwe?
6Jinsi watu wa Esau wanavyotafutwatafutwa! Jinsi hazina zake zilizofichwa zinavyoulizwaulizwa!
7Watu wote wa mapatano yako
Wamekufukuza, hadi mipakani;
Wale waliofanya amani nawe
Wamekudanganya, na kukushinda;
Walao mkate wako wameweka mtego chini yako;
Wala hana ufahamu wa hayo ndani yake.
8Siku hiyo, je! Sitawaangamiza watu wenye akili katika Edomu, na wenye ufahamu katika kilima cha Esau? Asema BWANA.
9Na mashujaa wako, Ee Temani, watafadhaika, hata iwe kila mtu akatiliwe mbali kwa kuuawa katika kilima cha Esau.[#Zab 76:5; Yer 49:22; Amo 2:16; Nah 3:13]
10Kwa sababu ya udhalimu aliotendwa ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika, nawe utakatiliwa mbali hata milele.[#Mwa 47:21; Zab 137:7; Eze 35:5,15; Amo 1:11; Mal 1:4]
11Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpigia kura Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao.[#Nah 3:10]
12Lakini usiitazame siku ya ndugu yako, siku ya mashaka yake, wala usisimange juu ya wana wa Yuda siku ya kuangamizwa kwao; wala usinene maneno ya kiburi katika siku ya shida yao.[#Mik 4:11; Mit 24:17]
13Usiingie katika lango la watu wangu, siku ya msiba wao; naam, usiyatazame mateso yao, siku ya msiba wao; wala usitie mikono yako juu ya mali zao, siku ya msiba wao.
14Wala usisimame penye njia panda, ili kuwakatilia mbali watu wake wakimbiao; wala usiwatoe watu wake waliosalia, katika siku ya dhiki.[#Isa 34:5-17; 63:1-6; Yer 49:7-22; Eze 25:12-14; 35:1-15; Amo 1:11-12; Mal 1:2-5]
15Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.[#Amu 1:7; Zab 137:8; Eze 35:15; Yoe 3:7,8]
16Kwa maana kama vile mlivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, ndivyo mataifa yote watakavyokunywa daima; naam, watakunywa na kuyumbayumba, nao watakuwa kana kwamba hawakuwa kamwe.
17Bali katika mlima Sayuni kutakuwa na watakaookoka, nao utakuwa mtakatifu; na nyumba ya Yakobo watamiliki tena milki zao.
18Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa muali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa BWANA amesema hayo.
19Na watu wa Negebu wataumiliki mlima wa Esau; na watu wa Shefela watawamiliki Wafilisti; nao wataimiliki nchi ya Efraimu, na nchi ya Samaria, na Benyamini atamiliki Gileadi.[#Sef 2:7]
20Na watu wa jeshi hili la wana wa Israeli waliotekwa, walio kati ya Wakanaani, watamiliki mpaka Sarepta; na hao watu wa Yerusalemu waliotekwa, waliomo Sefaradi, wataimiliki miji ya Negebu.[#1 Fal 17:9]
21Tena waokoaji watakwea juu ya mlima Sayuni ili kuuhukumu mlima wa Esau; na huo ufalme utakuwa ni mali ya BWANA.[#Isa 19:20; Dan 2:24; Zek 14:9; Ufu 11:15]