The chat will start when you send the first message.
1Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;
Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.
2Hazina za uovu hazifaidii kitu;[#Zab 49:6; Lk 12:19; Dan 4:27]
Bali haki huokoa na mauti.
3BWANA hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa;[#Zab 10:14]
Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.
4Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini;[#Mit 13:4]
Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.
5Akusanyaye wakati wa joto ni mwana mwenye hekima;
Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.
6Baraka humkalia mwenye haki kichwani;[#Est 7:8]
Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.
7Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka;[#Zab 9:5,6; Mhu 8:10]
Bali jina la mtu mwovu litaoza.
8Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo;
Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
9Aendaye kwa unyofu huenda salama;[#Zab 23:4; Isa 33:15,16]
Bali apotoshaye njia zake atajulikana.
10Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko;
Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
11Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima;[#Zab 37:30; 107:42]
Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,
12Kuchukiana huleta fitina;[#Yak 5:20; 1 Pet 4:8; 1 Kor 13:4]
Bali kupendana husitiri makosa yote.
13Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu;[#Lk 4:22]
Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.
14Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa;
Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.
15Mali ya tajiri ndio ngome yake;[#Ayu 31:24; Mit 18:11; Lk 12:19; 1 Tim 6:17]
Ufukara wa maskini ndio umwangamizao.
16Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima;
Mazao ya wabaya huielekea dhambi.
17Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima;
Bali yeye aachaye maonyo hukosa.
18Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo,
Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.
19Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu;[#Mhu 5:3; Zab 39:1; Mit 17:27,28; Yak 1:19]
Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.
20Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha safi;
Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.
21Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi;
Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.
22Baraka ya BWANA hutajirisha,[#Mwa 12:2; Kum 8:17,18; 1 Sam 2:7,8; 1 Tim 4:8]
Wala hachanganyi huzuni nayo.
23Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo;
Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.
24Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia;[#Ayu 15:21; Mt 5:6]
Na wenye haki watapewa matakwa yao.
25Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena;[#Zab 15:5; Mt 7:24; 1 Tim 6:19]
Bali mwenye haki ni msingi wa milele.
26Kama siki menoni, na kama moshi machoni,
Ndivyo alivyo mtu mvivu kwa hao waliomwajiri.
27Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu;[#Mhu 7:17]
Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.
28Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha;[#Zab 16:9; Rum 5:2; Ayu 8:13]
Bali matarajio yao wasio haki yatapotea.
29Njia ya BWANA ni kimbilio lake mtu mkamilifu;[#Zek 10:12; Flp 4:13; Isa 40:31; Zab 1:6]
Bali ni uharibifu kwao watendao maovu.
30Mwenye haki hataondolewa milele;
Bali wasio haki hawatakaa katika nchi.
31Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima;
Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali.
32Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa;
Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.