The chat will start when you send the first message.
1Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa rafiki yako,[#Mwa 43:9; Mit 27:13; Ebr 7:22; Ezr 10:19]
Ikiwa wewe na mgeni mmepeana mikono,
2Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako,
Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,
3Sasa, mwanangu, fanya hivi ukajiokoe,
Kwa kuwa umejitia mkononi mwa jirani yako;
Nenda ukanyenyekee, na kumsihi jirani yako.
4Usiache macho yako kupata usingizi,[#Rut 3:18]
Wala kope za macho yako kusinzia.
5Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji,
Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego.
6Ewe mvivu, mwendee chungu,[#Ayu 12:7]
Zitafakari njia zake ukapate hekima.
7Kwa maana yeye hana kiongozi,
Wala msimamizi, wala mkuu,
8Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua;
Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.
9Ewe mvivu, utalala hadi lini?
Utaondoka lini katika usingizi wako?
10Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,[#Mit 24:33-34]
Bado kukunja mikono upate usingizi!
11Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi,
Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.
12Mtu asiyefaa kitu, mtu wa uovu;
Huenda njiani mwenye kinywa cha upotovu.
13Hukonyeza kwa macho, hunena kwa miguu,[#Zab 35:19; Mit 10:10]
Huwaashiria watu kwa vidole vyake.
14Mna upotovu moyoni mwake, hutunga uovu daima,[#Zab 36:4; Isa 32:7; Mik 2:1; Mt 26:4]
Hupanda mbegu za magomvi.
15Basi msiba utampata kwa ghafla;[#Yer 19:11]
Ghafla atavunjika, bila njia ya kupona.
16Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA;
Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake.
17Macho ya kiburi, ulimi wa uongo,[#Zab 5:6; Mit 12:22; Hos 4:1,2; Yn 8:44; Mit 1:11; Isa 1:15]
Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;
18Moyo uwazao mawazo mabaya;[#Mwa 6:5; Isa 59:7; Rum 3:15]
Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;
19Shahidi wa uongo asemaye uongo;[#Zab 27:12]
Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.
20Mwanangu, shika maagizo ya baba yako,[#Efe 6:1]
Wala usiiache sheria ya mama yako.
21Yafunge hayo katika moyo wako daima;
Jivike hayo shingoni mwako.
22Uendapo yatakuongoza, ulalapo yatakulinda,
Na uamkapo yatazungumza nawe.
23Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru,[#Zab 19:8]
Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima.
24Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate,
Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni.
25Usiutamani uzuri wake moyoni mwako;[#2 Sam 11:2-5; Mt 5:28]
Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake.
26Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate;[#Mit 29:3; Eze 13:18]
Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani
27Je! Mtu aweza kuchukua moto kifuani pake,
Na nguo zake zisiteketezwe?
28Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto,
Na nyayo zake zisiungue?
29Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake;
Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia.
30Watu hawamdharau mwizi,
Akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa;
31Lakini akipatikana, atalipa mara saba;[#Kut 22:1,4]
Atatoa mali yote ya nyumba yake.
32Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa;[#Ayu 31:12; Ebr 13:4]
Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.
33Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima;
Wala fedheha yake haitafutika.
34Maana wivu ni ghadhabu ya mtu;
Wala hatahurumia siku ya kujilipizia kisasi.
35Hatakubali fidia yoyote;
Wala hatakuwa radhi, ujapomlipa vitu vingi.