Mithali 9

Mithali 9

Karamu ya hekima

1Hekima ameijenga nyumba yake,[#Mt 16:18; Efe 2:20; 1 Tim 3:15; Ebr 3:3-6]

Amezichonga nguzo zake saba;

2Amechinja nyama zake, amechanganya divai yake,

Ameiandalia meza yake pia.

3Amewatuma wajakazi wake, analia,[#Mt 22:3,4,9; Lk 14:17; Rum 10:15]

Mahali pa mjini palipoinuka sana,

4Kila aliye mjinga na aingie humu.[#Mit 6:32; Mt 11:25]

Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,

5Njoo ule mkate wangu,[#Wim 5:1; Isa 55:1; Mt 26:26-28]

Ukanywe divai niliyoichanganya.

6Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi,

Mkaende katika njia ya ufahamu.

7Amkemeaye mwenye dharau hujipatia fedheha;

Amkaripiaye mtu mbaya hujipatia aibu.

8Usimkaripie mwenye dharau, asije akakuchukia;[#Mt 7:6; Zab 141:5]

Mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda.

9Mwelimishe mwenye hekima, naye atazidi kuwa na hekima;[#Mt 13:12]

Mfundishe mwenye haki, naye atazidi kuwa na elimu;

10Kumcha BWANA ni mwanzo wa hekima;[#Ayu 28:28; Zab 111:10; Mit 1:7]

Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu.

11Maana, kwa msaada wangu siku zako zitazidishwa;[#Mit 10:27]

Na miaka ya maisha yako itaongezwa.

12Kama una hekima, una hekima kwa nafsi yako;[#Ayu 35:6,7]

Na kama una dharau, utaichukua peke yako.

13Mwanamke mpumbavu hupiga kelele,

Ni mjinga, hajui kitu.

14Hukaa mlangoni pa nyumba yake,

Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka,

15Apate kuwaita wapitao njiani,

Waendao moja kwa moja katika njia zao.

16Kila aliye mjinga na aingie humu.

Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,

17Maji yaliyoibiwa ni matamu,[#Mit 20:17]

Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza.

18Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo;

Ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya