Zaburi 102

Zaburi 102

Sala ya kutaka msaada kutoka kwa Mungu

1Ee BWANA, usikie kuomba kwangu,

Kilio changu kikufikie.

2Usinifiche uso wako siku ya shida yangu,

Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi.

3Maana siku zangu zinatoweka kama moshi,[#Yak 4:14; Omb 1:13]

Na mifupa yangu inateketea kama kinga.

4Moyo wangu umepigwa kama majani na kukauka,

Naam, ninasahau kula chakula changu.

5Kwa ajili ya kilio cha kuugua kwangu

Mifupa yangu imegandamana na nyama yangu.

6Nimekuwa kama ndege wa jangwani,[#Isa 34:11; Sef 2:14]

Na kufanana na bundi katika mahame.

7Nakesha, tena nimekuwa kama shomoro

Aliye peke yake juu ya nyumba.

8Adui zangu wananilaumu mchana kutwa;[#Mdo 23:12]

Wanaonichukia kana kwamba wana wazimu

Wakitaja jina langu katika laana zao.

9Maana ninakula majivu kama chakula,

Na kukichanganya kinywaji changu na machozi.

10Kwa sababu ya ghadhabu yako na hasira yako;[#Zab 30:7]

Maana umeniinua na kunitupilia mbali.

11Siku zangu ni kama kivuli cha jioni,[#Yak 1:10]

Nami ninanyauka kama majani.

12Bali Wewe, BWANA utaketi ukimiliki milele,[#1 Tim 6:16]

Na jina lako litakumbukwa na vizazi vyote.

13Wewe mwenyewe utasimama,[#Isa 40:2]

Na kuirehemu Sayuni,

Kwa maana ndio wakati wa kuihurumia,

Naam, majira yaliyoamriwa yamewadia.

14Maana watumishi wako wameyaridhia mawe yake,[#Dan 9:2]

Na kuyaonea huruma mavumbi yake.

15Kisha mataifa wataliogopa jina la BWANA,[#1 Fal 8:43]

Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;

16BWANA atakapokuwa ameijenga Sayuni,

Atakapoonekana katika utukufu wake,

17Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,[#Neh 2:8]

Asiyadharau maombi yao.

18Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,[#Rum 15:4; 1 Kor 10:11; Zab 22:31; Isa 43:21]

Na watu watakaoumbwa watamsifu BWANA.

19Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,[#Kum 26:15; Zab 14:2]

Toka mbinguni BWANA ameiangalia nchi,

20Ili akisikie kilio cha kuugua kwake aliyefungwa,

Na kuwafungua walioandikiwa kufa.

21Watu walitangaze jina la BWANA katika Sayuni,

Na sifa zake katika Yerusalemu,

22Pindi mataifa watapokusanyika pamoja,[#Hos 1:11]

Na falme, ili kumtumikia BWANA.

23Amezipunguza nguvu zangu njiani;

Amezifupisha siku zangu.

24Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu;[#Zab 90:2; Hab 1:12; Ufu 1:4,8]

Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi.

25Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi,[#Mwa 1:1; Kut 20:11; Ayu 38:4-7; Ebr 1:10-12]

Na mbingu ni kazi ya mikono yako.

26Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu[#Isa 66:22; Rum 8:20; 2 Pet 3:7]

Naam, hizi zitachakaa kama nguo;

Na kama mavazi utazibadilisha,

Nazo zitabadilika.

27Lakini Wewe U Yeye yule;[#Mal 3:6]

Na miaka yako haina mwisho.

28Wana wa watumishi wako watakaa,

Na wazawa wao wataimarishwa mbele zako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya