The chat will start when you send the first message.
1Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
2Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
3Akusamehe maovu yako yote,[#Isa 33:24; Mt 9:2; Mk 2:5; Lk 7:47; Kut 15:26; Yer 17:14]
Akuponya magonjwa yako yote,
4Aukomboa uhai wako kutoka kwa kaburi,
Akutia taji la fadhili na rehema,
5Aushibisha mema uzee wako,
Ujana wako ukarejezwa kama tai;
6BWANA ndiye afanyaye mambo ya haki,
Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
7Alimjulisha Musa njia zake,
Wana wa Israeli matendo yake.
8BWANA amejaa huruma na neema,[#Kut 34:6; Hes 14:18; Kum 5:10; Yak 5:11]
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
9Yeye hatashutumu daima,[#Isa 57:16; Yer 3:5; Mik 7:18]
Wala hatashika hasira yake milele.
10Hakututenda kulingana na hatia zetu,[#Ezr 9:13]
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
11Maana, kama mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Ndivyo fadhili zake zilivyo kuu kwa wamchao.
12Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,[#Isa 43:25; Efe 1:7]
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
13Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake,[#Kum 8:5; Isa 63:15,16; Mal 3:17]
Ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao.
14Kwa maana Yeye anatujua umbo letu,
Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.
15Mwanadamu siku zake zi kama majani;
Kama ua la kondeni ndivyo anavyostawi.
16Maana upepo hupita juu yake, na kutoweka!
Lisionekane mahali lilipokuwa tena.
17Bali fadhili za BWANA ni kwa wamchao[#Kut 20:6]
Tangu milele hata milele,
Na haki yake ni kwa vizazi vyote;
18Kwa wale walishikao agano lake,[#Kum 7:9]
Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye.
19BWANA ameweka kiti chake cha enzi mbinguni,[#Zab 47:2]
Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.
20Mhimidini BWANA, enyi malaika zake,[#Mt 6:10]
Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake,
Mkiisikiliza sauti ya neno lake.
21Mhimidini BWANA, enyi majeshi yake yote,[#Mwa 32:2; Dan 7:9]
Ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.
22Mhimidini BWANA, enyi matendo yake yote,
Mahali pote pa milki yake.
Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA.