The chat will start when you send the first message.
1Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA.
Wewe, BWANA, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Umejivika heshima na utukufu.
2Umejivika nuru kama vazi;
Umezitandika mbingu kama pazia;
3Na kuziweka nguzo za ghorofa zake majini.[#Amo 9:6; Isa 19:1]
Huyafanya mawingu kuwa gari lake,
Na kwenda juu ya mabawa ya upepo,
4Huwafanya malaika zake kuwa pepo,[#Ebr 1:7]
Na watumishi wake kuwa moto wa miali.
5Uliiweka nchi juu ya misingi yake,
Isitikisike milele.
6Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi,
Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima.
7Kwa kukemea kwako yakakimbia,
Kwa sauti ya radi yako yakaenda zake kasi,
8Yakapanda milima, yakateremka mabondeni,[#Ayu 38:10]
Mpaka mahali ulipoyatengenezea.
9Umeweka mpaka yasiupite,[#Ayu 26:10; Zab 33:7; Yer 5:22; Mwa 9:11]
Wala yasirudi kuifunikiza nchi.
10Hupeleka chemchemi katika mabonde;
Zapita kati ya milima;
11Zamnywesha kila mnyama wa porini;
Kwayo punda mwitu huzima kiu yao.
12Kandokando hukaa ndege wa angani;
Na kuimba wakiwa katika matawi.
13Huinywesha milima toka juu angani;
Nchi umeitosheleza kwa mazao ya kazi zako.
14Huyameesha majani kwa makundi,[#Mwa 1:29,30; Zab 147:8; 136:25; Ayu 28:5]
Na maboga kwa matumizi ya mwanadamu;
Ili atoe chakula katika nchi,
15Na divai imfurahishe mtu moyo wake.[#Amu 9:13; Mit 31:6,7; Mhu 10:19; Yer 31:12; Mit 14:23; Yn 2:9,10]
Aung'aze uso wake kwa mafuta,
Na mkate umburudishe mtu moyo wake.
16Miti ya BWANA nayo imetoshelezwa maji,[#Hes 24:6; Zab 29:5]
Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17Humo ndege hujenga viota vyao,
Korongo, anayo makao katika misonobari.
18Milima mirefu ndiko waliko mbuzi wa mwitu,[#Mit 30:26]
Na magenge ni kimbilio lao wibari.
19Aliufanya mwezi kwa ajili ya nyakati,[#Mwa 1:14; Ayu 38:12]
Jua latambua kuchwa kwake.
20Wewe hufanya giza, kukawa usiku,[#Isa 45:7]
Ndipo atambaapo kila mnyama wa mwitu.
21Wanasimba hunguruma wakitaka mawindo,[#Ayu 38:39]
Wakitafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.
22Jua linapochomoza, wanakwenda zao,
Na kujilaza mapangoni mwao.
23Mwanadamu atoka kwenda zake kazini,[#Mwa 3:19]
Na kwenye utumishi wake mpaka jioni.
24Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako![#Mwa 1:20-22]
Kwa hekima umevifanya vyote pia.
Dunia imejaa viumbe wako.
25Bahari iko kule, kubwa na upana,
Ndimo mlimo viendavyo visivyohesabika,
Viumbe hai wakubwa kwa wadogo.
26Ndimo zipitamo merikebu,[#Ayu 41:1; Zab 74:14; Isa 27:1]
Ndimo alimo Lewiathani uliyemwumba acheze humo.
27Hao wote wanakungoja Wewe,[#Rum 11:36]
Uwape chakula chao kwa wakati wake.
28Wewe huwapa,
Wao wanakiokota;
Wewe waukunjua mkono wako,
Wao wanashiba mema;
29Wewe wauficha uso wako,[#Mhu 12:7]
Wao wanafadhaika;
Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
30Waituma roho yako, wanaumbwa,[#Isa 32:15]
Nawe waufanya upya uso wa nchi.
31Utukufu wa BWANA na udumu milele;
BWANA na ayafurahie matendo yake.
32Aitazamaye nchi, ikatetemeka;[#Hab 3:10]
Aigusaye milima, ikatoka moshi.
33Nitamwimbia BWANA maadamu ninaishi;
Nitamshangilia Mungu wangu nikiwa hai;
34Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Maana furaha yangu hutoka kwa BWANA.
35Wenye dhambi waangamizwe katika nchi,[#Mit 2:22]
Watendao ubaya wasiwepo tena.
Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA.