The chat will start when you send the first message.
1Haleluya.[#Isa 12:4; #105:1 maana yake ni, Msifuni BWANA.]
Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake,
Wajulisheni watu matendo yake.
2Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Yasimulieni maajabu yake yote.
3Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA.
4Mtafuteni BWANA na nguvu zake,[#Zab 27:8]
Utafuteni uso wake sikuzote.
5Yakumbukeni matendo yake ya ajabu aliyoyafanya,[#Kum 8:2]
Miujiza yake na hukumu alizotoa.
6Enyi wazawa wa Abrahamu, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
7Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu;[#Isa 26:9]
Hukumu zake ziko duniani kote.
8Analikumbuka agano lake milele;[#Lk 1:72]
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
9Agano alilofanya na Abrahamu,[#Mwa 12:7; 17:8; 26:3]
Na ahadi yake kwa Isaka.
10Alilomthibitishia Yakobo liwe amri,[#Mwa 28:13]
Na Israeli liwe agano la milele.
11Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani,[#Mwa 15:18]
Kama fungu la urithi wenu.
12Walipokuwa watu wawezao kuhesabiwa,[#Mwa 34:30; Kum 7:7; Mwa 17:8; Ebr 11:9]
Naam, watu wachache na wageni katika nchi,
13Wakatangatanga toka taifa hadi taifa,
Toka ufalme mmoja hadi kwa watu wengine.
14Hakumwacha mtu awaonee,[#Mwa 12:17; 20:3-7; 35:5]
Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao.
15Akisema, Msiwaguse masihi wangu,[#105:15 Au, mtiwa mafuta.]
Wala msiwadhuru nabii zangu.
16Akasababisha njaa katika nchi,[#Mwa 41:53-57; 2 Fal 8:1; Law 26:26]
Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
17Alimpeleka mtu mbele yao,[#Mwa 37:28; 45:5]
Yusufu aliuzwa utumwani.
18Walimwumiza miguu yake kwa pingu,[#Mwa 39:20—40:15,23]
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
19Hadi wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya BWANA ilimjaribu.
20Mfalme alituma watu na kumfungua,[#Mwa 41:14]
Mkuu wa watu akamwachilia huru.
21Akamweka kuwa mkuu wa nyumba yake,[#Mwa 41:39-41]
Na mwenye mamlaka juu ya mali yake yote.
22Awaongoze maofisa wake kama apendavyo,
Na kuwafundisha wazee wake hekima.
23Israeli naye akaingia Misri,[#Mwa 46:6; 47:11]
Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu.
24Akawajalia watu wake wazae sana,[#Kut 1:7-14; Kum 26:5; Mdo 7:17]
Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao.
25Akawageuza moyo wawachukie watu wake,
Wakawatendea hila watumishi wake.
26Akamtuma Musa, mtumishi wake,[#Kut 3:10—4:17; Hes 16:5]
Na Haruni ambaye amemchagua.
27Akatenda mambo ya ishara zake kati yao,
Na miujiza katika nchi ya Hamu.
28Alituma giza, na kufanya nchi kuwa na giza,[#Kut 10:21-23; Zab 99:7]
Wakayaasi maneno yake.
29Aliyageuza maji yao yakawa damu,[#Kut 7:17-21]
Akawaua samaki wao.
30Nchi yao ilijaa vyura,[#Kut 8:1-6]
Hata nyumbani mwa wafalme wao.
31Alisema, kukaja makundi ya mainzi,[#Kut 8:16-17,20-24]
Na chawa katika nchi yao yote.
32Badala ya mvua aliwapa mvua ya mawe,[#Kut 9:22-25]
Na umeme uliomulika ghafla katika nchi yao.
33Akaipiga mizabibu yao na mitini yao,
Akaivunja miti ya nchi yao.
34Alisema, kukaja nzige,[#Kut 10:12-15]
Na tunutu wasiohesabika;
35Wakaila miche yote ya nchi yao,
Wakayala matunda ya ardhi yao.
36Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi,[#Mwa 49:3; Kut 12:29]
Malimbuko ya nguvu zao.
37Akawatoa wakiwa na fedha na dhahabu,[#Kut 12:33-36]
Katika makabila yao asiwepo mwenye kujikwaa.
38Misri ilifurahi walipoondoka,
Maana kwa ajili yao hofu imewaangukia.
39Alitandaza wingu liwe kifuniko,[#Kut 13:21-22; Neh 9:12]
Na moto ili uwaangazie usiku.
40Walimwomba naye akaleta kware,[#Kut 16:2-15]
Na kuwashibisha chakula cha mbinguni.
41Akaufunua mwamba, kukabubujika maji,[#Kut 17:1-7; Hes 20:2-13; Neh 9:15; Isa 48:21; 1 Kor 10:4]
Yakapita jangwani kama mto.
42Maana alilikumbuka neno lake takatifu,
Na Abrahamu, mtumishi wake.
43Akawatoa watu wake kwa shangwe,
Na wateule wake kwa nyimbo za furaha.
44Akawapa nchi za mataifa, wakairithi kazi ya watu;[#Kum 6:10; Yos 11:16-23; 13:7]
45Ili wazishike amri zake, na kuzitii sheria zake.[#Kum 4:1]
Haleluya.