Zaburi 106

Zaburi 106

Ungamo la dhambi za Israeli

1Haleluya.[#1 Nya 16:34; 2 Nya 5:13; 7:3; Ezr 3:11; Zab 100:5; 107:1; 118:1; 136:1; Isa 63:7; Yer 33:11; Mt 19:17]

Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema,

Kwa maana fadhili zake ni za milele.

2Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya BWANA,[#Zab 40:5]

Au kuzihubiri sifa zake zote?

3Heri washikao hukumu,[#Yer 22:15,16; Mt 22:37; Zab 15:2; Mdo 24:16; Gal 6:9]

Na kutenda haki sikuzote.

4Ee BWANA, unikumbuke mimi,

Kwa kibali ulicho nacho kwa watu wako.

Unijie kwa wokovu wako,

5Ili niuone wema wa wateule wako.

Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako,

Na kujisifu pamoja na watu wako.

6Tumetenda dhambi pamoja na baba zetu,[#Law 26:40; 1 Fal 8:47; Dan 9:5]

Tumetenda maovu, tumefanya ubaya.

7Baba zetu katika Misri[#Kut 14:10-12]

Hawakuzingatia matendo yako ya ajabu;

Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako;

Wakaasi penye bahari, Bahari ya Shamu.

8Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake,[#Yos 7:9; Zab 143:11; Yer 14:7,21]

Ayadhihirishe matendo yake makuu.

9Akaikemea Bahari ya Shamu ikakauka,[#Kut 14:21-31; Nah 1:4; Isa 63:11]

Akawaongoza vilindini kana kwamba ni nchi kavu.

10Akawaokoa kutoka kwa mkono wa mtu adui, aliyewachukia,

Na kuwakomboa kutoka kwa mkono wa adui zao.

11Maji yakawafunika watesi wao,

Hakusalia hata mmoja wao.

12Ndipo walipoyaamini maneno yake,[#Kut 15:1-21]

Waliziimba sifa zake.

13Lakini punde wakayasahau matendo yake,

Wakakosa kungojea ushauri wake.

14Bali walitamani sana nyikani,[#Hes 11:4-34]

Wakamjaribu Mungu jangwani.

15Akawapa walichomwomba,[#Isa 10:16]

Lakini akawatumia ugonjwa wa kuwakondesha.

16Wakamhusudu Musa kambini,[#Hes 16:1-35]

Na Haruni, mtakatifu wa BWANA.

17Nchi ikapasuka ikammeza Dathani,

Ikaufunika mkutano wa Abiramu.

18Moto ukawaka katika mkutano wao,

Miali yake ikawateketeza waovu.

19Walifanya ndama huko Horebu,[#Kut 32:1-14]

Wakaisujudia sanamu ya kusubu.

20Wakaubadili utukufu wao[#Yer 2:11; Rum 1:23]

Kuwa mfano wa ng'ombe mla majani.

21Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,

Aliyetenda makuu katika Misri.

22Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,

Mambo ya kutisha penye Bahari ya Shamu.

23Akasema ya kuwa atawaangamiza[#Kut 32:10; Kum 9:19; Eze 13:5; 20:13]

Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,

Mbele zake na kusimama palipobomoka,

Ili aigeuze hasira yake asije akawaangamiza.

24Wakaidharau nchi ile ya kupendeza,[#Hes 14:1-35]

Wala hawakuliamini neno lake.

25Bali wakanung'unika hemani mwao,

Wala hawakuisikiliza sauti ya BWANA.

26Ndipo alipowainulia mkono wake na kuwaapia,

Ya kuwa atawaangamiza jangwani,

27Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa,[#Law 26:33]

Na kuwatapanya katika nchi mbali.

28Wakamwabudu Baal-Peori,[#Hes 25:1-13; Kum 4:3; Hos 9:10; Ufu 2:14]

Wakazila dhabihu zilizotolewa kwa wafu.

29Wakamkasirisha kwa matendo yao;

Tauni ikawashambulia.

30Ndipo Finehasi akasimama akafanya hukumu;

Tauni ikazuiliwa.

31Akahesabiwa kuwa ana haki

Kizazi baada ya kizazi hata milele.

32Wakamghadhabisha penye maji ya Meriba,[#Hes 20:2-13; Yak 3:2]

Hasara ikampata Musa kwa ajili yao,

33Kwa sababu waliiasi roho yake,

Akasema yasiyofaa kwa midomo yake.

34Hawakuwaangamiza watu wa nchi[#Amu 1:21; 2:1-3; 3:5-6; Kum 7:2]

Kama BWANA alivyowaambia;

35Bali walijichanganya na mataifa,[#Amu 3:5; Isa 2:6]

Wakajifunza matendo yao.

36Wakazitumikia sanamu zao,[#Kut 23:33; Kum 7:10; Amu 2:12; 2 Fal 17:8-11; 2 Nya 33:2-7]

Nazo zikawa mtego kwao.

37Naam, walitoa wana wao na binti zao[#Kum 12:30,31; Isa 57:5; Eze 16:20; 2 Fal 17:17]

Kuwa dhabihu kwa mashetani.

38Wakamwaga damu isiyo na hatia,[#Hes 35:33]

Damu ya wana wao na binti zao,

Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani;

Nchi ikatiwa unajisi kwa damu.

39Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao,

Wakafanya uasherati kwa matendo yao.

40Hasira ya BWANA ikawaka juu ya watu wake,[#Amu 2:14-18]

Akauchukia urithi wake.

41Akawatia mikononi mwa mataifa,[#Amu 2:14; Neh 9:27]

Nao waliowachukia wakawatawala.

42Adui zao wakawaonea,

Wakatiishwa chini ya mkono wao.

43Mara nyingi aliwaponya,

Bali walikuwa wakimwasi kwa mashauri yao,

Wakawa dhalili kwa uovu wao.

44Lakini aliyaangalia mateso yao,[#Amu 10:10]

Aliposikia kilio chao.

45Akawakumbukia agano lake;[#Law 26:41; Omb 3:32]

Akawahurumia kwa wingi wa fadhili zake;

46Akawajalia kuhurumiwa[#Ezr 9:9; Yer 42:12]

Na watu wote waliowateka.

47Ee BWANA, Mungu wetu, utuokoe,[#1 Nya 16:35-36; Lk 1:74; 2 Kor 5:15]

Utukusanye kwa kututoa katika mataifa,

Tulishukuru jina lako takatifu,

Tuzifanyie shangwe sifa zako.

48Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli,

Tangu milele hata milele.

Watu wote na waseme, Amina.

Haleluya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya