Zaburi 107

Zaburi 107

KITABU CHA TANO

Shukrani kwa kukombolewa katika dhiki

1Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema,[#1 Nya 16:34; 2 Nya 5:13; 7:3; Ezr 3:11; Zab 100:5; 106:1; 118:1; 136:1; Yer 33:11; Mt 19:17]

Kwa maana fadhili zake ni za milele.

2Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA,

Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi.

3Akawakusanya kutoka nchi zote,[#Zab 106:47; Isa 49:12; Yer 29:14; Eze 39:27]

Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.

4Walitangatanga jangwani katika njia ya nyika;

Hawakuona mji wa kukaa.

5Waliona njaa na kiu,

Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao.

6Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,[#Zab 50:15; Isa 41:17; Yer 29:12-14; Hos 5:15]

Akawaponya na shida zao.

7Akawaongoza kwa njia ya kunyoka,[#Ezr 8:21; Isa 63:12]

Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa.

8Na wamshukuru BWANA, kwa fadhili zake,

Na maajabu yake kwa wanadamu.

9Maana hushibisha nafsi yenye shauku,[#Zab 34:10; Isa 55:1; Mt 5:6; Lk 1:53]

Na nafsi yenye njaa huijaza mema.

10Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti,[#Ayu 36:8]

Wamefungwa katika taabu na minyororo,

11Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu,[#Omb 3:42; Zab 73:24; Lk 7:30; Mdo 20:27]

Wakalidharau shauri lake Aliye Juu.

12Hata akawadhili moyo kwa taabu,[#Isa 63:5]

Wakajikwaa, wala pasiwe na wa kuwasaidia.

13Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,

Akawaponya kutoka kwa shida zao.

14Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti,[#Zab 146:7; Mdo 12:7]

Akaivunja minyororo yao.

15Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake,

Na maajabu yake kwa wanadamu.

16Maana ameivunja milango ya shaba,[#Isa 45:2]

Ameyakata mapingo ya chuma.

17Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao,[#Zab 14:1; Mit 1:22; Omb 3:39]

Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa.

18Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula,

Wameyakaribia malango ya mauti.

19Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,

Akawaponya kutoka kwa shida zao.

20Hulituma neno lake, huwaponya,[#Hes 21:8; 2 Fal 20:4; Mt 8:8]

Huwatoa katika maangamizo yao.

21Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake,

Na maajabu yake kwa wanadamu.

22Na wamtolee dhabihu za kushukuru,[#Law 7:12; Zab 50:14; Ebr 13:15]

Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba.

23Washukao baharini katika merikebu,

Wafanyao kazi yao katika maji mengi,

24Hao huziona kazi za BWANA,

Na maajabu yake vilindini.

25Maana alisema, akavumisha upepo wa dhoruba,

Ukayainua juu mawimbi ya bahari.

26Walirushwa juu mbinguni, waliteremka hadi vilindini,[#Zab 22:14; Isa 13:7; Nah 2:10]

Uhodari wao ukayeyuka katika maafa yao.

27Waliyumbayumba, walipepesuka kama mlevi,

Ujuzi wao wote uliwaishia.

28Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,

Akawaponya kutoka kwa shida zao.

29Huituliza dhoruba, ikawa shwari,[#Zab 65:7; Isa 50:2; Mt 8:26; Mk 4:39-41]

Mawimbi yake yakanyamaza.

30Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia

Naye akawaleta mpaka bandani waliyoitamani.

31Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake,

Na maajabu yake kwa wanadamu.

32Na wamtukuze katika kusanyiko la watu,

Na wamhimidi katika baraza la wazee.

33Amegeuza mito ikawa jangwa,[#1 Fal 17:1; Isa 34:9,10; Eze 30:12; Yoe 1:20; Nah 1:4]

Na chemchemi za maji zikawa nchi kavu.

34Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi,[#Mwa 13:10]

Kwa sababu ya uovu wa wakazi wake.

35Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji,[#Isa 41:18]

Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji.

36Maana amewakalisha huko wenye njaa,[#Mdo 17:26]

Nao wamejenga mji wa kukaa.

37Wakapanda mbegu katika mashamba,

Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake.

38Naye aliwabariki wakaongezeka sana,[#Mwa 12:2]

Wala hawapunguzi mifugo wao.

39Walipopungua na kudhilika,[#2 Fal 10:32; Ayu 12:21]

Kwa kuonewa na dhiki na huzuni.

40Aliwamwagia wakuu dharau,

Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia.

41Lakini alimwinua mhitaji juu mbali na mateso,[#1 Sam 2:8; 2 Sam 7:8; Ayu 8:7]

Na kuwaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo.

42Wanyofu wa moyo wanaona na kufurahi,[#Ayu 22:19; 5:16; Mit 10:11]

Na waovu wote wananyamazishwa.

43Aliye na hekima na ayaangalie hayo;[#Yer 9:12; Dan 12:10]

Na wazitafakari fadhili za BWANA.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya