Zaburi 111

Zaburi 111

Sifa kwa maajabu ya Mungu

1Haleluya.[#111:1 maana yake ni, Msifuni BWANA.]

Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote,

Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.

2Matendo ya BWANA ni makuu,[#Ayu 38:1]

Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.

3Kazi yake imejaa heshima na adhama,

Na haki yake yadumu milele.

4Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;

BWANA ni mwenye fadhili na rehema.

5Amewapa wamchao chakula;

Atalikumbuka agano lake milele.

6Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake,

Kwa kuwapa urithi wa mataifa.

7Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,[#Zab 19:7]

Maagizo yake yote ni amini,

8Yamethibitika milele na milele,[#Ufu 15:3]

Yamefanywa kwa uaminifu na haki.

9Amewapelekea watu wake ukombozi,[#Ufu 15:3]

Ameamuru agano lake liwe la milele,

Jina lake ni takatifu na la kuogopwa.

10Kumcha BWANA ndio mwanzo wa hekima,[#Kum 4:6; Ayu 28:28; Mit 1:7; 9:10; Mhu 12:3]

Wote wafanyao hayo wana ufahamu mzuri,

Sifa zake zadumu milele.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya