Zaburi 115

Zaburi 115

Unyonge wa sanamu na ukuu wa Mungu

1Ee BWANA, kutukuza usitutukuze sisi,[#Isa 48:11; Eze 36:32]

Bali ulitukuze jina lako,

Kwa ajili ya fadhili zako,

Kwa ajili ya uaminifu wako.

2Kwa nini mataifa kusema,[#Zab 42:3,10; 79:10; Yoe 2:17]

Yuko wapi Mungu wao?

3Lakini Mungu wetu yuko mbinguni,[#1 Nya 16:26; Zab 135:6; Dan 4:35]

Alitakalo lote amelitenda.

4Sanamu zao ni fedha na dhahabu,[#Kum 4:28; Zab 135:15-18; Isa 40:19; Yer 20:3; Hos 8:6; 1 Kor 10:19,20; Ufu 9:20]

Kazi ya mikono ya wanadamu.

5Zina vinywa lakini hazisemi,

Zina macho lakini hazioni,

6Zina masikio lakini hazisikii,

Zina pua lakini hazinusi harufu,

7Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi,

Wala hazitoi sauti kwa koo zake.

8Wazitengenezao watafanana nazo,[#Zab 135:18; Isa 44:9,10; Yon 2:8; Hab 2:18]

Sawa na wote wanaozitumainia.

9Enyi Israeli, mtumainini BWANA;[#Zab 33:20; Mit 30:5]

Yeye ni msaada wao na ngao yao.

10Enyi mlango wa Haruni, mtumainini BWANA;[#Mal 2:7]

Yeye ni msaada wao na ngao yao.

11Enyi mmchao BWANA, mtumainini BWANA;

Yeye ni msaada wao na ngao yao.

12BWANA ametukumbuka,[#Efe 1:3]

Naye atatubariki sisi.

Ataubariki mlango wa Israeli,

Ataubariki mlango wa Haruni,

13Atawabariki wamchao BWANA,[#Law 26:3; Kum 11:27; Zab 24:4; Mit 10:6; Ufu 11:18; 19:5]

Wadogo kwa wakubwa.

14BWANA na awaongeze ninyi,

Ninyi na watoto wenu.

15Na mbarikiwe ninyi na BWANA,[#Mwa 14:19; 1:1; Zab 96:5]

Aliyezifanya mbingu na nchi.

16Mbingu ni mbingu za BWANA,

Bali nchi amewapa wanadamu.

17Wafu hawamsifu Mungu BWANA,

Wala yeyote ashukaye kwenye kimya;

18Bali sisi tutamhimidi BWANA,[#Zab 145:2; Dan 2:20]

Tangu leo na hata milele.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya