Zaburi 135

Zaburi 135

Sifa kwa wema na ukuu wa Mungu

1Haleluya.

Lisifuni jina la BWANA,

Enyi watumishi wa BWANA, sifuni.

2Ninyi msimamao nyumbani mwa BWANA,[#Lk 2:37]

Nyuani mwa nyumba ya Mungu wenu.

3Msifuni BWANA kwa kuwa BWANA ni mwema,

Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza.

4Kwa sababu BWANA amejichagulia Yakobo,[#Kut 19:5; Kum 7:6,7]

Na Israeli, wawe watu wake hasa.

5Maana najua ya kuwa BWANA ni mkuu,

Na Bwana wetu yuko juu ya miungu yote.

6BWANA amefanya kila lililompendeza,

Katika mbingu na katika nchi,

Katika bahari na katika vilindi vyote.

7Ndiye apandishaye mvuke toka miisho ya nchi;[#Mwa 2:6; Ayu 5:10; Yer 10:13; Zek 10:1; Ayu 28:25; 38:22]

Huifanyia mvua umeme;

Hutoa upepo katika ghala zake.

8Aliwapiga wazaliwa wa kwanza wa Misri,

Wa wanadamu na wa wanyama.

9Alituma ishara na maajabu kati yako, Ee Misri,

Juu ya Farao na watumishi wake wote.

10Aliwapiga mataifa mengi,[#Hes 21:24]

Akawaua wafalme wenye nguvu;

11Sihoni, mfalme wa Waamori,[#Yos 12:7]

Na Ogu, mfalme wa Bashani,

Na falme zote za Kanaani.

12Akaitoa nchi yao iwe urithi,[#Mwa 17:8]

Urithi wa Israeli watu wake.

13Ee BWANA, jina lako linadumu milele,[#Kut 3:15]

BWANA, sifa zako zitakumbukwa na vizazi vyote.

14Kwa kuwa BWANA atawaamua watu wake,[#Kum 32:36]

Na kuwahurumia watumishi wake.

15Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu,[#Zab 115:4-8; Ufu 9:20]

Kazi ya mikono ya wanadamu.

16Zina vinywa lakini hazisemi,

Zina macho lakini hazioni,

17Zina masikio lakini hazisikii,

Wala hamna pumzi vinywani mwake.

18Wazifanyao watafanana nazo,

Na kila mmoja anayezitumainia.

19Enyi mlango wa Israeli, mhimidini BWANA;

Enyi mlango wa Haruni, mhimidini BWANA;

20Enyi mlango wa Lawi, mhimidini BWANA;

Ninyi mnaomcha BWANA, mhimidini BWANA.

21Na ahimidiwe BWANA toka Sayuni,

Akaaye Yerusalemu.

Haleluya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya