Zaburi 138

Zaburi 138

Shukrani na sifa ya Daudi

1Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,[#Zab 119:46]

Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.

2Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,[#1 Fal 8:29; Zab 5:7; Dan 6:10; Yon 2:7; Isa 42:21]

Nitalishukuru jina lako,

Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,

Kwa maana umeikuza ahadi yako,

na jina lako juu ya vyote.

3Siku ile niliyokuita uliniitikia,[#2 Kor 12:9; Zek 10:12]

Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.

4Ee BWANA, wafalme wote wa dunia watakushukuru,

Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.

5Naam, wataziimba njia za BWANA,

Kwa maana utukufu wa BWANA ni mkuu.

6Ingawa BWANA yuko juu, anamjali mnyenyekevu,[#Mit 3:34; Yak 4:6]

Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.

7Nijapopitia katika shida,[#Zab 23:3]

Unanilinda juu ya hasira ya adui zangu,

Unaunyosha mkono wako,

Na mkono wako wa kulia unaniokoa.

8BWANA atanitimizia malengo yake kwangu;[#Zab 57:2; Flp 1:6]

Ee BWANA, fadhili zako ni za milele;

Usiiache kazi ya mikono yako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya