Zaburi 140

Zaburi 140

Sala ya ukombozi kutoka kwa adui

1Ee BWANA, uniokoe kutoka kwa watu waovu.

Unihifadhi kutoka kwa watu wajeuri.

2Waliowaza mabaya mioyoni mwao,

Kila siku huchochea vita.

3Wamenoa ndimi zao na kuwa kama za nyoka,[#Rum 3:13]

Na katika midomo yao mna sumu ya fira.

4Ee BWANA, unilinde Kutoka kwa mikono ya mtu asiye haki;

Unihifadhi na watu wajeuri;

Waliopanga kuniangusha.

5Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba;[#Zab 10:9; Yer 18:22; Lk 11:53-54]

Wametandika wavu kando ya njia;

Wameniwekea matanzi.

6Nimemwambia BWANA, Ndiwe Mungu wangu;[#Zab 16:2]

Ee BWANA, uisikie sauti ya dua zangu.

7Ee MUNGU Bwana, nguvu za wokovu wangu,[#Kum 33:27-29; Zab 18:32]

Umenifunika kichwa changu siku ya vita.

8Ee BWANA, usimpe asiye haki tamaa zake,[#Ayu 5:12,13]

Usiifanikishe hila yake, wasije wakajiinua.

9Nao wainuapo vichwa watu wanaonizunguka,[#Zab 7:16]

Madhara ya midomo yao yawafunike.

10Makaa ya moto yawaangukie, watupwe motoni,[#Zab 11:6]

Na katika mashimo, wasipate kusimama tena.

11Msingiziaji hatawekwa imara katika nchi,

Mtu wa jeuri, uovu humwinda kumwangamiza.

12Najua ya kuwa BWANA atamfanyia mnyonge hukumu,[#Zab 109:31]

Na wahitaji haki yao.

13Hakika wenye haki watalishukuru jina lako,

Wenye adili watakaa mahali ulipo Wewe.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya