Zaburi 143

Zaburi 143

Sala ya ukombozi kutoka kwa adui

1Ee BWANA, uisikie sala yangu, uzisikilize dua zangu Unijibu Kwa uaminifu wako,

Unijibu kwa haki yako.

2Wala usimhukumu mtumishi wako,[#Ayu 14:3; 4:17; Mhu 7:20; Rum 3:20; Gal 2:16]

Maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki.

3Maana adui ameifuatia nafsi yangu,[#Zab 7:1-2]

Ameutupa chini uzima wangu.

Amenikalisha mahali penye giza,

Kama watu waliokufa zamani.

4Na roho yangu imezimia ndani yangu,[#Zab 61:2]

Moyo wangu ndani yangu umeshtuka.

5Nimezikumbuka siku za kale,[#Zab 77:5,11]

Nimeyatafakari matendo yako yote,

Naziwaza kazi za mikono yako.

6Nakunyoshea mikono yangu;[#Zab 28:2]

Nafsi yangu inakuonea kiu kama nchi kame.

7Ee BWANA, unijibu hima, roho yangu imelegea;

Usinifiche uso wako,

Nisifanane nao washukao shimoni.

8Uniwezeshe kusikia fadhili zako asubuhi,

Kwa maana nimekutumaini Wewe.

Unifundishe njia nitakayoiendea,

Kwa maana ninakuinulia nafsi yangu.

9Ee BWANA, uniponye kutoka kwa adui zangu;

Nimekukimbilia Wewe, unifiche.

10Unifundishe kuyatenda mapenzi yako,[#Zab 25:4; Yn 14:26; Rum 5:5; Efe 4:30; Gal 5:22-23]

Kwa maana ndiwe Mungu wangu;

Roho yako mwema aniongoze katika njia iliyo sawa,

11Ee BWANA, uniponye kwa ajili ya jina lako,

Kwa haki yako unitoe roho yangu taabuni;

12Kwa fadhili zako utawakatilia mbali adui zangu;

Na kuwaangamiza wote wanitesao nafsi,

Kwa maana mimi ni mtumishi wako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya