Zaburi 144

Zaburi 144

Sala kwa ukombozi wa kitaifa na usalama

1Na ahimidiwe BWANA, mwamba wangu,[#2 Sam 22:35]

Aifundishaye mikono yangu vita,

Na vidole vyangu kupigana.

2Mwamba wangu na ngome yangu,[#144:2 Au Mhisani.]

Nguzo yangu na mwokozi wangu

Ngao yangu ninayemkimbilia,

Huwatiisha watu wangu chini yangu.

3Ee BWANA, mtu ni kitu gani hata umjali?[#Ayu 7:17-18; Zab 8:4; Ebr 2:6]

Na binadamu hata umwangalie?

4Binadamu ni kama ubatili,

Siku zake ni kama kivuli kipitacho.

5Ee BWANA, uziinamishe mbingu zako, ushuke chini.[#Isa 64:1]

Uiguse milima ili nayo itoe moshi.

6Utupe umeme, uwatawanye,

Uipige mishale yako, uwafadhaishe.

7Uinyoshe mikono yako toka juu, uniponye,[#Zab 69:1; Mal 2:11]

Unitoe katika maji mengi, kutoka kwa mkono wa wageni,

8Vinywa vyao vinasema visivyofaa,

Na ambao mikono yao ya kulia ni ya uongo.

9Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,[#Zab 33:2]

Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.

10Awapaye wafalme wokovu,

Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu.

11Uniponye, unitoe,

Katika mkono wa wageni.

Vinywa vyao vyasema visivyofaa,

Na mkono wao wa kulia ni mkono wa uongo.

12Wavulana wetu wakiwa ujanani wawe kama miche

Iliyostawi kikamilifu.

Binti zetu wawe kama nguzo za pembeni

Zilizochongwa ili kupamba kasri.

13Ghala zetu na zijae

Zenye akiba za jinsi zote.

Kondoo zetu na wazae

Elfu na makumi elfu mashambani mwetu.

14Ng'ombe wetu na wabebe mizigo mizito,[#Law 26:17]

Kusiwe na kushambuliwa.

Wala kusiwe na kuhamishwa,

Wala malalamiko katika njia zetu.

15Heri watu wenye hali hiyo,[#Kum 33:29]

Heri watu wenye BWANA kuwa Mungu wao.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya