Zaburi 145

Zaburi 145

Ukuu na wema wa Mungu

1Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza,

Nitalihimidi jina lako milele na milele.

2Kila siku nitakuhimidi,

Nitalisifu jina lako milele na milele.

3BWANA ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana,

Wala ukuu wake hauchunguziki.

4Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako,

Kitayatangaza matendo yako makuu.

5Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako,

Na matendo yako yote ya ajabu.

6Watu watayataja matendo yako ya kutisha,

Nami nitausimulia ukuu wako.

7Watasimulia juu ya ukuu wa wema wako mwingi.

Na wataiimba haki yako kwa sauti.

8BWANA ni mwenye fadhili na huruma,[#Kut 34:6; Hes 14:18; Zab 86:5,15; 57:10; Omb 3:22,23; Yn 1:17]

Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,

9BWANA ni mwema kwa watu wote,[#Zab 100:5; Nah 1:7; Mt 5:45; Mdo 14:17]

Na rehema zake ziko juu ya vyote alivyoumba.

10Ee BWANA, kazi zako zote zitakushukuru,[#Zab 19:1]

Na wacha Mungu wako watakuhimidi.

11Wataunena utukufu wa ufalme wako,

Na kusena uweza wako.

12Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,

Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.

13Ufalme wako ni ufalme wa milele,

BWANA ni mwaminifu katika maneno yake yote,

Na mwenye fadhili katika matendo yake yote

Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.

14BWANA huwategemeza wote waangukao,

Huwainua wote walioinama chini.

15Macho ya watu wote yakuelekea Wewe,

Nawe huwapa chakula chao wakati wake.

16Waufumbua mkono wako,

Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.

17BWANA ni mwenye haki katika njia zake zote,

Na mwenye huruma katika matendo yake yote.

18BWANA yuko karibu na wote wamwitao,[#Zab 91:1; Isa 61:10; Yn 14:23; Yak 4:8; 1 Yoh 2:24; Yud 1:23; Ufu 3:20; Yn 4:24]

Wote wamwitao kwa uaminifu.

19Hutimiza matakwa ya wote wamchao,[#1 Yoh 5:14]

Na pia husikia kilio chao, na huwaokoa.

20BWANA huwahifadhi wote wampendao,[#1 Pet 1:5]

Na wote wasio haki atawaangamiza.

21Kinywa changu kitazinena sifa za BWANA;

Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu

milele na milele.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya