Zaburi 146

Zaburi 146

Sifa kwa kupata msaada wa Mungu

1Haleluya.[#146:1 maana yake ni, Msifuni BWANA.]

Ee nafsi yangu, umsifu BWANA.

2Nitamsifu BWANA muda ninaoishi,

Nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai.

3Msiwatumainie wakuu,[#Isa 2:22]

Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake.

4Pumzi yake inapomtoka, anarudi katika udongo wake,[#Mhu 12:7; 1 Kor 2:6]

Siku iyo hiyo mipango yake hutoweka.

5Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,[#Yer 17:7]

Na tumaini lake ni kwa BWANA, Mungu wake,

6Aliyezifanya mbingu na nchi,[#Mik 7:20; Mdo 4:24; 14:15; Ufu 14:7]

Bahari na vitu vyote vilivyomo.

Huishika kweli milele,

7Huwafanyia hukumu walioonewa,

Huwapa wenye njaa chakula;

BWANA hufungua waliofungwa;

8BWANA huwafumbua macho waliopofuka;

BWANA huwainua walioinama;

BWANA huwapenda wenye haki;

9BWANA huwahifadhi wageni;

Huwategemeza yatima na mjane;

Bali njia ya wasio haki huiharibu.

10BWANA atamiliki milele,

Mungu wako, Ee Sayuni, kwa vizazi vyote.

Haleluya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya