Zaburi 27

Zaburi 27

Wimbo wa ushindi katika Bwana wa Daudi

1BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu,

Nimwogope nani?

BWANA ni ngome ya uzima wangu,

Nimhofu nani?

2Watenda mabaya waliponikaribia,

Wanile nyama yangu,

Watesi wangu na adui zangu,

Walijikwaa wakaanguka.

3Jeshi lijapojipanga kupigana nami,

Moyo wangu hautaogopa.

Vita vijaponitokea,

Hata hapo nitatumainia BWANA.

4Neno moja nimelitaka kwa BWANA,

Nalo ndilo nitakalolitafuta,

Nikae nyumbani mwa BWANA

Siku zote za maisha yangu,

Niutazame uzuri wa BWANA,

Na kutafakari hekaluni mwake.

5Maana atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya,[#Mit 18:10; Isa 4:6; Kol 3:3]

Atanisitiri katika sitara ya hema yake,

Na kuniinua juu ya mwamba.

6Na sasa kichwa changu kitainuka

Juu ya adui zangu wanaonizunguka.

Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake;

Nitaimba, naam, nitamhimidi BWANA.

7Ee BWANA, usikie, kwa sauti yangu ninalia,

Unifadhili, unijibu.

8Uliposema, “Nitafuteni uso wangu,”

Moyo wangu umekuambia,

BWANA, uso wako nitautafuta.

9Usinifiche uso wako,

Usimkatalie mtumishi wako kwa hasira.

Umekuwa msaada wangu, usinitupe,

Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.

10Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha,[#Isa 49:15; Yn 16:32; 2 Tim 4:16-18]

Bali BWANA atanikaribisha kwake.

11Ee BWANA, unifundishe njia yako,

Na kuniongoza katika njia iliyonyoka;

Kwa sababu yao wanaoniotea;

12Usinitie katika nia ya watesi wangu;[#1 Sam 22:9; Mt 26:59,60]

Maana mashahidi wa uongo wamenijia,

Nao watoao jeuri kama pumzi.

13Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA[#Zab 112:7,8]

Katika nchi ya walio hai.

14Umtumainie BWANA, uwe imara,[#Zab 62:1,5; Isa 25:9; Hab 2:3]

Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya