The chat will start when you send the first message.
1Nimekukimbilia Wewe, BWANA,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye,
2Unitegee sikio lako, uniokoe hima.[#Zab 71:2; Mit 22:17]
Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
Ngome thabiti ya kuniokoa.
3Ndiwe mwamba wangu na ngome yangu;[#Zab 23:3; Yer 14:7]
Kwa ajili ya jina lako uniongoze na unichunge.
4Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana Wewe ndiwe ngome yangu.
5Mikononi mwako naiweka roho yangu;[#Lk 23:46; Mdo 7:59; 2 Tim 1:12; Ebr 6:18]
Umenikomboa, Ee BWANA, Mungu wa kweli.
6Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo;
Bali mimi namtumainia BWANA.
7Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako,[#Yn 10:27]
Kwa kuwa umeyaona mateso yangu.
Umeijua nafsi yangu taabuni,
8Wala hukunitia mikononi mwa adui;[#Zab 18:19]
Miguu yangu umeisimamisha mahali penye usalama.
9Ee BWANA, unifadhili, maana ni katika dhiki,
Jicho langu limenyauka kwa masumbufu,
Naam, mwili wangu na nafsi yangu.
10Maana maisha yangu yamekwisha kwa huzuni,
Na miaka yangu kwa maumivu.
Nguvu zangu zimeniishia kwa uovu wangu,
Na mifupa yangu imepooza.
11Kwa sababu ya watesi wangu nimelaumiwa,[#Zab 88:8]
Naam, hasa kwa jirani zangu;
Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu;
Wanaoniona njiani wananikimbia.
12Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa;
Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.
13Maana nimesikia wengi wakinong'onezana;[#Yer 20:3; Omb 2:22; Mt 27:1]
Hofu katika pande zote.
Waliposhauriana juu yangu,
Walipanga kunitoa uhai wangu.
14Lakini mimi nakutumaini Wewe, BWANA,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
15Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye kutoka kwa adui zangu na wanaonifuatia.
16Umwangaze mtumishi wako[#Hes 6:25; Zab 4:6; Dan 9:17]
Kwa nuru ya uso wako;
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
17Ee BWANA, nisiaibishwe, maana nimekuita;[#Zab 25:2]
Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni.
18Midomo ya uongo iwe na ububu,[#Zab 12:3]
Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi,
Kwa majivuno na dharau.
19Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako[#Isa 64:4; 1 Kor 2:9]
Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao
Mbele ya wanadamu!
20Utawasitiri kutoka kwa fitina za watu[#Zab 27:5; Ayu 5:21]
Katika maficho ya kuwapo kwako;
Utawaficha katika hema
Na ushindani wa ndimi.
21BWANA ahimidiwe; kwa maana amenitendea
Fadhili za ajabu nilipozongwa kama mji wenye boma.
22Nami nilisema kwa pupa yangu,
Nimekatiliwa mbali na macho yako;
Lakini ulisikia sauti ya kilio changu
Wakati nilipokulilia.
23Mpendeni BWANA,[#1 Pet 1:5]
Ninyi nyote mlio watauwa wake.
BWANA huwahifadhi waaminifu,
Bali humlipiza mwenye kiburi ipasavyo.
24Iweni hodari, na mpige moyo konde,
Ninyi nyote mnaomngoja BWANA.