Zaburi 38

Zaburi 38

Ombi la uponyaji kwa anayejuta kwa mateso

1Ee BWANA, usinilaumu katika ghadhabu yako,

Wala usiniadhibu kwa ukali wa hasira yako.

2Kwa maana mishale yako imenichoma,

Na mkono wako umenipata.

3Hamna uzima katika mwili wangu

Kwa sababu ya ghadhabu yako.

Wala hamna amani mifupani mwangu

Kwa sababu ya hatia zangu.

4Maana dhambi zangu zimenifunika kichwa,

Kama mzigo mzito zimenilemea mno.

5Majeraha yangu yananuka na kutunga usaha,

Kwa sababu ya upumbavu wangu.

6Nimejipinda na kuinama sana,

Mchana kutwa ninaenda nikiomboleza.

7Maana viuno vyangu vimejaa homa,[#Ayu 7:5]

Wala hamna uzima katika mwili wangu.

8Nimedhoofika na kupondeka sana,

Nimeugua kwa fadhaa ya moyo wangu.

9Bwana, haja zangu zote ziko mbele zako,

Kuugua kwangu hakukusitirika kwako.

10Moyo wangu unadundadunda,

Nguvu zangu zimenitoka;

Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka.

11Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu;[#Lk 10:31]

Na jamaa zangu wanasimama mbali.

12Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego;

Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya;

Na kufikiri hila mchana kutwa.

13Lakini kama kiziwi sisikii,

Nami ni kama bubu asiyefumbua kinywa chake.

14Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia,

Ambaye hamna ubishi kinywani mwake.

15Kwa kuwa nakungoja Wewe, BWANA,[#Yer 14:8]

Wewe utajibu, Ee Bwana, Mungu wangu.

16Maana nilisema, Wasije wakanifurahia;

Wale wanaojitukuza juu yangu Mguu wangu unapoteleza.

17Kwa maana mimi ni karibu na kusita,

Na maumivu yangu yako mbele yangu daima.

18Kwa maana nitaungama uovu wangu,[#Ayu 31:33; Zab 32:5; Mit 28:13; 2 Kor 7:9]

Na kusikitika kwa dhambi zangu.

19Lakini walio adui zangu bila sababu wana nguvu,

Nao wanaonichukia bure wamekuwa wengi.

20Naam, wakilipa mabaya kwa mema,[#1 Yoh 3:12; 1 Pet 3:13]

Huwa adui zangu kwa kuwa nilifuata lililo jema.

21Wewe, BWANA, usiniache,[#Zab 22:1,11]

Mungu wangu, usijitenge nami.

22Ufanye haraka kunisaidia,[#Kut 15:2; Isa 12:2]

Ee Bwana, wokovu wangu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya