Zaburi 39

Zaburi 39

Sala ya kutaka hekima na msamaha

1Nilisema, Nitazitunza njia zangu[#1 Fal 2:4; Mit 4:26,27; Ebr 2:1; Kol 4:5]

Nisije nikakosa kwa ulimi wangu;

Nitajitia lijamu kinywani,

Maadamu mtu mbaya awapo mbele yangu.

2Nilikuwa sisemi, nilinyamaa kimya,

Sina faraja, maumivu yangu yakazidi.

3Moyo wangu ukawa moto ndani yangu,[#Yer 20:9]

Na katika kuwaza kwangu moto ukawaka;

Nilisema kwa ulimi wangu,

4BWANA, unijulishe mwisho wangu,

Na idadi ya siku zangu ni ngapi;

Nijue jinsi maisha yangu yalivyo mafupi.

5Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri;[#Zab 90:4]

Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako.

Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili.

6Kweli, watu wote hupita kama kivuli;

Wao hujisumbua bure tu;

Wanajirundikia mali wala hawajui ni nani atakayeirithi.

7Na sasa ninangoja nini, Ee Bwana?

Matumaini yangu ni kwako.

8Uniokoe kutoka kwa maasi yangu yote,

Usinifanye niwe wa kulaumiwa na mpumbavu.

9Nimenyamaza, sifumbui kinywa changu,

Maana Wewe ndiwe uliyeyafanya.

10Uniondolee pigo lako;

Kwa mapigo ya mkono wako nimeangamia.

11Ukimrudi mtu kwa kumkemea kwa uovu wake,

Watowesha uzuri wake kama nondo.

Kila mwanadamu ni ubatili.

12Ee BWANA, usikie maombi yangu,[#Law 25:23; 1 Nya 29:15]

Utege sikio lako niliapo,

Usiyapuuze machozi yangu.

Kwa maana mimi ni mgeni wako,

Msafiri kama baba zangu wote.

13Uache kunitazama, ndio nipate kufurahi tena,[#Ayu 10:20,21]

Kabla sijafa na kutoweka kabisa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya