The chat will start when you send the first message.
1Nilimngoja BWANA kwa subira,
Akaniinamia na kusikia kilio changu.
2Akanipandisha toka shimo la uharibifu,
Toka udongo wa utelezi;
Akaisimamisha miguu yangu mwambani,
Akaziimarisha hatua zangu.
3Akatia wimbo mpya kinywani mwangu,
Ndio sifa zake Mungu wetu.
Wengi wataona na kuogopa,
Nao watamtumainia BWANA.
4Heri aliyemfanya BWANA kuwa tumaini lake,[#Zab 2:12]
Wala hakuwaelekea wenye kiburi,
Wala hao wanaogeukia uongo.
5Ee BWANA, Mungu wangu, umefanya kwa wingi[#Isa 55:8]
Miujiza yako na mawazo yako kwetu;
Hakuna awezaye kufananishwa nawe;
Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri,
Ni mengi sana hayahesabiki.
6Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,[#Ebr 10:5-7; Hos 6:6; Mt 9:13]
Umetuzidishia ila masikio,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
7Ndipo niliposema, Tazama nimekuja,[#Lk 24:44; Yn 5:39; Mdo 10:43; Ebr 10:7]
(Katika gombo la kitabu nimeandikiwa,)
8Kuyafanya mapenzi yako,[#Ayu 23:12; Yer 15:16; Yn 4:34; Rum 7:22]
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.
9Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa.[#Zab 139:2]
Sikuizuia midomo yangu; Ee BWANA, unajua.
10Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;[#Mdo 20:20; Rum 1:16,17; Flp 3:9]
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyiko kubwa.
11Nawe, BWANA, usinizuilie rehema zako,[#Zab 43:3]
Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima.
12Kwa maana mabaya yasiyohesabika[#Zab 38:4]
Yamenizunguka mimi.
Maovu yangu yamenipata,
Wala siwezi kuona.
Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu,
Nami nimevunjika moyo.
13Ee BWANA, uwe radhi kuniokoa,
Ee BWANA, unisaidie hima.
14Waaibike na wafedheheke,
Wote wanaotaka kuniua.
Warudishwe nyuma, watahayarishwe,
Wapendezwao na shari yangu.
15Wafadhaike kwa aibu yao,
Wanaoniambia Ewe! Ewe!
16Washangilie na wakufurahie,
Wote wakutafutao.
Waupendao wokovu wako
Waseme daima, BWANA ni Mkuu.
17Nami ni maskini na mhitaji,[#Neh 5:19; Yon 1:6]
Bwana atanitunza.
Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu,
Ee Mungu wangu, usikawie.