Zaburi 45

Zaburi 45

Wimbo wa arusi ya kifalme

1Moyo wangu umefurika kwa jambo jema,

Mimi nasema niliyomfanyia mfalme;

Ulimi wangu ni kama kalamu ya mwandishi stadi.

2Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu;

Neema imemiminiwa midomoni mwako,

Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele.

3Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari,

Utukufu ni wako na fahari ni yako.

4Katika fahari yako usitawi uendelee

Kwa ajili ya kweli, upole na haki

Na mkono wako wa kulia

Utakutendea mambo ya ajabu.

5Mishale yako ni mikali, katika mioyo ya adui za mfalme;

Watu huanguka chini yako.

6Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele,[#Ebr 1:8-9; Zab 93:2; Isa 9:6,7]

Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.

7Umeipenda haki;[#Zab 33:5; Mt 3:15; Ebr 1:9; Isa 61:1; Yn 20:17]

Umeichukia dhuluma.

Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekutia mafuta,

Mafuta ya furaha kuliko wenzako.

8Mavazi yako yote hunukia manemane

Na udi na mdalasini.

Katika majumba ya pembe

Vinubi vimekufurahisha.

9Binti za wafalme wamo

Miongoni mwa akina bibi wako wastahiki.

Katika mkono wako wa kulia amesimama malkia

Akiwa amevaa dhahabu safi ya Ofiri.

10Sikia, binti, utazame, utege sikio lako,[#Kum 21:13]

Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.

11Naye mfalme atautamani uzuri wako,[#Zab 95:6; Isa 54:5]

Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.

12Na watu wa Tiro wanakushawishi kwa zawadi,[#45:12 Katika Kiebrania ni binti Tiro.]

Nao matajiri wa watu watajipendekeza kwako.

13Binti mfalme yumo ndani ana fahari tupu,[#Ufu 19:7,8]

Mavazi yake ni ya nyuzi za dhahabu.

14Anapelekwa kwa mfalme

Na mavazi yaliyofumwa kwa uzuri.

Wanawali wenzake wanaomfuata,

Pia watapelekwa kwako.

15Watapelekwa kwa furaha na shangwe,

Na kuingia katika nyumba ya mfalme.

16Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako,[#1 Pet 2:9; Ufu 1:6]

Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote.

17Jina lako nitalifanya kuwa kumbukumbu[#Isa 11:10; Mal 1:11]

Katika vizazi vyote.

Kwa hiyo mataifa watakushukuru

Milele na milele.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya