Zaburi 50

Zaburi 50

Ibada ya kweli

1Mungu, Mungu BWANA, amenena, ameiita nchi,

Toka maawio ya jua hadi machweo yake.

2Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri,

Mungu ameangaza kote.

3Mungu wetu atakuja wala sio kimya kimya,

Moto utakula mbele zake,

na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote.

4Ataziita mbingu zilizo juu,[#Mik 6:1,2]

Na nchi pia, ili awahukumu watu wake.

5Nikusanyieni wacha Mungu wangu[#Isa 13:3; 1 Kor 6:2; 1 The 3:13; Yud 1:14; Kut 24:7; Isa 59:20,21; Ebr 8:6]

Waliofanya agano nami kwa dhabihu.

6Na mbingu zitatangaza haki yake,

Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.

7Sikieni, enyi watu wangu, nami nitanena,

Mimi nitakushuhudia, Israeli;

Mimi ndimi niliye MUNGU, Mungu wako.

8Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,

Na kafara zako ziko mbele zangu daima.

9Sitatwaa ng'ombe katika nyumba yako,[#Isa 43:23; Mik 6:6; Mdo 17:25]

Wala beberu katika mazizi yako.

10Maana kila mnyama-pori ni wangu,

Na mifugo juu ya angani elfu.

11Nawajua ndege wote wa milima,

Na wanyama wote wa mashamba ni wangu.

12Kama ningekuwa na njaa singekuambia,

Maana ulimwengu ni wangu, na vyote vilivyomo.

13Je! Nile nyama ya mafahali!

Au ninywe damu ya mbuzi!

14Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru;[#Hes 14:2]

Mtimizie Aliye Juu nadhiri zako.

15Uniite siku ya mateso;[#Ayu 22:27; Zab 22:23; Mt 5:16; Yn 15:8]

Nitakuokoa, nawe utanitukuza.

16Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia,

Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,

Na kuliweka agano langu kinywani mwako?

17Maana wewe umechukia maonyo,[#Mit 1:7; 5:12,13; Rum 2:21; 2 The 2:10-12]

Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

18Ulipomwona mwizi ulikuwa radhi naye,[#Rum 1:32]

Ukashirikiana na wazinzi.

19Umekiachia kinywa chako kinene mabaya,

Na ulimi wako unatunga uongo.

20Umekaa na kumsengenya ndugu yako,

Na mwana wa mama yako umemsingizia.

21Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza;[#Mhu 8:11; Rum 2:4]

Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.

Lakini nitakukemea;

Nitakuhukumu kwa hayo yote.

22Yafahamuni hayo,

Ninyi mnaomsahau Mungu,

Nisije nikawararueni,

Asipatikane wa kuwaokoa.

23Atoaye dhabihu za kushukuru,

Ndiye anayenitukuza.

Naye autengenezaye mwenendo wake,

Nitamwonesha wokovu wa Mungu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya