Zaburi 58

Zaburi 58

Sala ya kutaka kisasi

1Ni kweli, enyi wakuu, mnanena haki?

Enyi wanadamu, mnahukumu kwa adili?

2Sivyo! Mioyoni mwenu mnatenda maovu;[#Zab 94:20]

Mikono yenu wenyewe inaeneza udhalimu katika nchi.

3Waovu hupotoka hata kabla ya kuzaliwa kwao;[#Zab 51:5]

Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.

4Wana sumu mfano wa sumu ya nyoka;[#Zab 140:4]

Wao ni kama fira kiziwi azibaye sikio lake.

5Asiyeisikiliza sauti ya waganga,

Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi.

6Ee Mungu, uyavunje meno yao vinywani mwao;[#Ayu 4:10]

Ee BWANA, uyavunje magego ya wanasimba.

7Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi;

Akiielekeza mishale yake, iwe imetiwa ubutu.

8Kama konokono ayeyukaye na kutoweka,

Kama mimba iliyoharibika, isiyoliona jua,

9Kabla ya masufuria yenu kupata moto wa miiba,[#Mit 10:25]

Ataipeperusha kama chamchela,

Iliyo mibichi na iliyo moto.

10Mwenye haki atafurahi akionapo kisasi;[#Kum 32:42; Ayu 22:19; Zab 18:47; Mit 10:11; Ufu 18:20]

Ataiosha miguu yake katika damu ya wasio haki.

11Na mwanadamu atasema,[#Rum 2:6-11; Ayu 34:11; Mhu 5:8; Yer 32:19; Eze 7:27; Rum 14:12; Ufu 2:23]

Hakika iko thawabu yake mwenye haki.

Hakika yuko Mungu

Anayehukumu katika dunia.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya