Zaburi 74

Zaburi 74

Ombi la kutaka msaada wakati wa kushindwa

1Ee Mungu, mbona umetutupa milele?[#Zab 95:7; Yer 23:1; Eze 34:8,31; Lk 12:32]

Kwa nini hasira yako inatoka moshi

Juu ya kondoo wa malisho yako?

2Ulikumbuke kusanyiko lako,

Ulilolinunua zamani.

Ulilolikomboa liwe kabila la urithi wako,

Mlima Sayuni ulioufanya maskani yako.

3Upite na kupaona palipoharibika milele;

Adui ameufanya kila ubaya katika patakatifu.

4Watesi wako wamenguruma kati ya kusanyiko lako;[#Dan 6:27]

Wameweka bendera zao ziwe alama.

5Wanaonekana kama watu wainuao mashoka,

Waikate miti ya msituni.

6Na sasa nakishi yake yote pia

Wanaivunjavunja kwa mashoka na nyundo.

7Wamepatia moto patakatifu pako;

Wamelinajisi kao la jina lako hata chini.

8Walisema mioyoni mwao,[#Zab 83:4]

Na tuwaangamize kabisa;

Mahali penye mikutano ya Mungu

Wamepachoma moto katika nchi pia.

9Hatuzioni ishara zetu, wala sasa hakuna nabii,[#1 Sam 3:1; Mik 3:6; Mt 16:4]

Wala kwetu hakuna ajuaye, hadi lini?

10Ee Mungu, mtesi atalaumu hata lini?

Adui alidharau jina lako hata milele?

11Mbona unaurudisha mkono wako,

Naam, mkono wako wa kulia,

Uutoe kifuani mwako,

Ukawaangamize kabisa.

12Lakini Mungu ni mfalme wangu tokea zamani,[#Zab 44:4]

Afanyaye mambo ya wokovu katikati ya nchi.

13Wewe umeipasua bahari kwa nguvu zako,[#Kut 14:21; Isa 51:9]

Umevivunja vichwa vya nyangumi juu ya maji.

14Wewe ulivivunja vichwa vya Lewiathani,[#Kut 17:5,6; Hes 14:9; Hes 20:11; Ayu 41:1; Isa 11:16; Isa 27:1; Yos 3:13; Zab 72:9; Zab 104:26; Zab 105:41; Hab 3:9; Ufu 16:12]

Awe chakula cha watu wa jangwani.

15Wewe ulitokeza chemchemi na kijito;

Wewe ulikausha mito yenye maji sikuzote.

16Mchana ni wako, usiku nao ni wako,

Ndiwe uliyeufanya mwanga na jua.

17Wewe uliiweka mipaka yote ya dunia,[#Mdo 17:26]

Majira ya joto na ya baridi wewe uliyafanya.

18Ee BWANA, uyakumbuke hayo, adui amelaumu,[#Ufu 16:19]

Na watu wapumbavu wamelidharau jina lako.

19Usimpe mnyama mkali uhai wa njiwa wako;[#Wim 2:14; 4:1]

Usiwasahau milele watu wako walioonewa.

20Ulitafakari agano lako;[#Mwa 17:7; Law 26:44; Yer 33:21]

Maana mahali kwenye giza katika nchi

Kumejaa makao ya ukatili.

21Aliyeonewa asirejee ametiwa haya,[#Zab 9:18]

Mnyonge na mhitaji na walisifu jina lako.

22Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe,[#Isa 37:23]

Ukumbuke unavyotukanwa na mpumbavu mchana kutwa.

23Usiisahau sauti ya watesi wako,

Ghasia yao wanaokupinga inapaa daima.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya