The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu, usistarehe,
Ee Mungu, usinyamae, wala usitulie.
2Maana adui zako wanafanya ghasia,[#Zab 2:1]
Nao wakuchukiao wameviinua vichwa vyao.
3Juu ya watu wako wanafanya hila,[#Zab 27:5; Kol 3:3]
Na kushauriana juu yao uliowaficha.
4Wamesema, Njoni, tuwakatilie mbali wasiwe taifa,[#2 Sam 10:6; 2 Nya 20:1]
Na jina la Israeli halitakumbukwa tena.
5Maana wanashauriana kwa moyo mmoja,
Juu yako wanafanyana agano.
6Hema za Edomu, na Waishmaeli,
Na Moabu, na Wahagari,
7Gebali, na Amoni, na Amaleki,
Na Filisti, nao wanaokaa Tiro,
8Ashuri naye amepatana nao,
Wamewasaidia wana wa Lutu.
9Uwatende kama ulivyowatenda Midiani, Sisera,[#Hes 31:7,8; Isa 9:4; Amu 4:6-22; 7:1-23]
Na Yabini, penye kijito cha Kishoni.
10Ambao waliangamizwa Endori;
Wakawa samadi juu ya nchi.
11Uwafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu,[#Amu 7:25; 8:12]
Na wakuu wao wote kama Zeba na Zalmuna.
12Ambao Walisema,
Na tutamalaki makao ya Mungu.
13Ee Mungu, uwafanye kama mavumbi ya kisulisuli,
Kama ya makapi mbele ya upepo,
14Kama moto uteketezao msitu,
Kama miali ya moto iiwashayo milima,
15Ndivyo utakavyowafuatia kwa tufani yako,
Na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako.
16Uzijaze nyuso zao fedheha;
Ili wapate kulitafuta jina lako, Ee BWANA.
17Waaibike, wafadhaike milele,
Naam, watahayarike na kupotea.
18Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA,
Ndiwe peke yako Uliye Juu, juu ya nchi yote.