Zaburi 85

Zaburi 85

Sala ya kupata fadhili za Mungu tena

1BWANA, umeiridhia nchi yako,[#Yer 30:18; Eze 39:25]

Umewarejesha mateka wa Yakobo.

2Umeusamehe uovu wa watu wako,

Umezisitiri hatia zao zote.

3Umeiondoa ghadhabu yako yote,

Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako.

4Mungu wa wokovu wetu, uturudishe,

Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu.

5Je! Utatufanyia hasira hata milele?

Utadumisha ghadhabu kizazi hadi kizazi?

6Je! Hutaki kurudi na kutuhuisha,[#Hab 3:2]

Ili watu wako wakufurahie?

7Ee BWANA, utuoneshe rehema zako,

Utupe wokovu wako.

8Na nisikie atakavyosema Mungu BWANA,[#Hab 2:1; Zek 9:10; 2 Pet 2:20]

Maana atawaambia watu wake amani,

Naam, na watauwa wake pia,

Bali wasiurudie upumbavu tena.

9Hakika wokovu wake uko karibu na wamchao,

Ndipo utukufu wake ukae katika nchi yetu.

10Fadhili na kweli zitakutana,[#Mik 7:20; Yn 1:17; Zab 72:2,3; Isa 32:17; Lk 2:14; Yn 14:27]

Haki na amani zitakumbatiana.

11Kweli itachipuka katika nchi,[#Isa 45:8; 2 Kor 5:14-21]

Haki itachungulia kutoka mbinguni.

12Naam, BWANA atatoa kilicho chema,[#Yak 1:17]

Na nchi yetu itatoa mazao yake.

13Haki itakwenda mbele zake,

Na kuzitayarishia hatua zake mapito.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya