Ufunuo 1

Ufunuo 1

Utangulizi na salamu

1Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaoneshe watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa malaika akamwonesha mtumwa wake Yohana;[#Dan 2:28,29]

2aliyelishuhudia neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu Kristo, yaani, mambo yote aliyoyaona.[#Ufu 6:9]

3Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati uko karibu.[#Ufu 22:7,10]

4Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi;[#Kut 3:14,15; Isa 41:4; Ufu 3:1; 4:5; 5:6]

5tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,[#Isa 55:4; 40:2; Zab 89:27,37; 130:8; Yn 18:37; Kol 1:18; Ebr 9:14; Ufu 3:14; 7:14; 19:16]

6na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.[#Kut 19:6; Ufu 5:10; 1 Pet 2:5,9; Isa 61:6]

7Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na makabila yote ya dunia yataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina.[#Dan 7:13; Mt 24:30; Mk 13:26; Lk 21:27; 23:27,28; 1 The 4:17; Zek 12:10-14; Yn 19:34,37]

8Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.[#Kut 3:14; Ufu 22:13; 4:8; 21:6; Isa 41:4]

Maono ya Kristo

9Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu.

10Nilikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,

11ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika kitabu, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.[#Ufu 2:8; 22:13]

12Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu;

13na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu kifuani[#Dan 7:13; 10:5; Eze 1:26; 8:2]

14Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama muali wa moto;[#Dan 7:9; 10:6; Ufu 2:18; 19:12]

15na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuri; na sauti yake kama sauti ya maji mengi.[#Eze 1:24; 43:2]

16Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kulia; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake.[#Amu 5:31; Ufu 2:12,16; 19:15]

17Nami nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,[#Isa 44:6; 48:12; Ufu 2:8; 22:13; Dan 8:18; 10:15-19]

18na aliye hai; nami nilikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.

19Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.[#Isa 48:6; Dan 2:29]

20Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.[#Mal 2:7; Dan 2:29]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya