The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto.[#Ufu 4:3; 5:2]
2Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kulia juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi.
3Naye akaita kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.[#Yer 25:30; Hos 11:10; Amo 1:2]
4Na ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nilikuwa tayari kuandika. Nami nilisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie mhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike.[#Dan 8:26; 12:4,9]
5Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kulia kuelekea mbinguni,[#Kut 20:11; Kum 32:40; Dan 12:7; Amo 3:7]
6akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na kukawia tena baada ya haya;[#Mwa 14:19,22; Neh 9:6; Kut 20:11; Zab 146:6; Ufu 6:11; Dan 12:7]
7isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowatangazia watumishi wake hao manabii.[#Amo 3:7; Dan 9:6,10; Zek 1:6; Mdo 3:21; Ufu 11:15; 17:17]
8Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Nenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.[#Eze 2:8—3:3]
9Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.[#Eze 2:8; 3:1-3]
10Nikakitwaa kile kitabu kidogo kutoka mkononi mwa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.
11Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.[#Yer 1:10; 25:30; Dan 3:4; 7:14]