Ufunuo 11

Ufunuo 11

Mashahidi wawili

1Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, na madhabahu, na hao wanaosujudu humo.[#Eze 40:3; Zek 2:1-2; 2 Kor 6:16]

2Na behewa lililo nje ya hekalu uliache nje wala usilipime, kwa maana Mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arubaini na miwili.[#Lk 21:24; Isa 63:18; Lk 21:24; Zab 79:1; Dan 8:10; Ufu 12:6,14; 13:5]

3Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, wakiwa wamevikwa magunia.

4Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi.[#Zek 4:3,11-14]

5Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa.[#2 Fal 1:10; 2 Sam 22:9; Yer 5:14]

6Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo.[#1 Fal 17:1; Kut 7:17-19,20; 1 Sam 4:8]

7Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua.[#Dan 7:3,7,21; Ufu 13:1,5-7; 17:8]

8Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulubiwa.[#Isa 1:9-10; Lk 13:34]

9Na watu wa hao jamaa na kabila na lugha na taifa waitazama mizoga yao siku tatu u nusu, wala hawaiachi mizoga yao kuwekwa kaburini.

10Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi.[#Zab 105:38]

11Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama kwa miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama.[#Eze 37:5,10; Mwa 15:12]

12Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama.[#2 Fal 2:11]

13Na katika saa ile palikuwa na tetemeko kuu la nchi, na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka; wanadamu elfu saba wakauawa katika tetemeko lile. Na waliobakia wakaingiwa na hofu, wakamtukuza Mungu wa mbingu.[#Ufu 6:12; 16:18; Eze 38:19,20; Dan 2:19]

14Ole wao, pigo la pili limekwisha pita, tazama pigo la tatu linakuja punde.[#Ufu 9:12; 12:12]

Tarumbeta ya saba

15Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele.[#Kut 15:18; Dan 2:44; 7:14,27; Zek 14:9; Oba 1:21; Zab 2:2; 10:16; 22:28]

16Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vya enzi vyao wakaanguka kifudifudi, wakamsujudia Mungu[#Ufu 4:4,10; 7:11]

17wakisema, Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umeutwaa uweza wako ulio mkuu, na kumiliki.[#Kut 3:14; Isa 41:4; Ufu 4:8; 18:8]

18Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na wa kuwapa thawabu yao watumishi wako manabii na watakatifu, na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi.[#Zab 2:1,5,12; 46:6; 99:1; 110:5; 115:13; Ufu 15:1; Rum 2:5; Amo 3:7; Zek 1:6; Dan 9:6,10; #11:18 katika Kigiriki ni ‘watumwa’.]

19Kisha hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la Agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua kubwa ya mawe.[#Ufu 4:5; 8:5; 15:5; 16:18,21; 1 Fal 8:1,6; 2 Nya 5:7; Kut 9:24; 19:16]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya