Ufunuo 12

Ufunuo 12

Mwanamke na joka

1Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji la nyota kumi na mbili.

2Naye alikuwa ana mimba, akilia, akiwa na uchungu na kuumwa katika kuzaa.[#Isa 66:7; Mik 4:10]

3Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, lilikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba.[#Dan 7:7]

4Na mkia wake unakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, limle mtoto wake.[#Dan 8:10]

5Naye akazaa mtoto wa kiume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hadi kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi.[#Isa 66:7; Zab 2:9; Ufu 19:15]

6Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini.[#Mt 2:13; Ufu 11:2,3]

Mikaeli amshinda joka

7Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika wake wakapigana na lile joka, lile joka nalo likapigana nao pamoja na malaika wake;[#Dan 10:13,21; 12:1; Yud 1:9]

8lakini hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.

9Lile joka kuu likatupwa, yule nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika wake wakatupwa pamoja naye.[#Mwa 3:1,14; Lk 10:18; Yn 12:31; Zek 3:1,2]

10Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.[#Ayu 1:9-11; Zek 3:1; Ufu 11:15; Lk 22:31]

11Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.[#Rum 8:37; Ufu 7:14]

12Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu akiwa na ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.[#Isa 44:23; 49:13]

Joka anapigana tena katika dunia

13Na joka lile lilipoona ya kuwa limetupwa katika nchi, lilimfuatia mwanamke yule aliyemzaa mtoto wa kiume.

14Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hadi mahali pake, hapo alishwapo kwa nyakati tatu na nusu, mbali na nyoka huyo.[#Dan 7:25; 12:7]

15Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, ili achukuliwe na mto ule.

16Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule lililoutoa lile joka katika kinywa chake.

17Joka likamkasirikia yule mwanamke, likaenda zake lifanye vita juu ya wazawa wake waliobakia, wanaozishika amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; nalo likasimama juu ya mchanga wa bahari.[#Ufu 13:7; 14:12; 19:10; 1 Yoh 5:10; Mwa 3:15]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya