Ufunuo 13

Ufunuo 13

Mnyama wa kwanza

1Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, alikuwa na pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya kukufuru.[#Dan 7:3,7; Ufu 11:7; 17:3,7-12]

2Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, lile joka likampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.[#Dan 7:4-6; Ufu 12:3]

3Nikaona mojawapo wa vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la mauti likapona. Dunia yote ikamstaajabia mnyama yule.[#Ufu 17:8]

4Wakalisujudu lile joka kwa sababu lilimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye?

5Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya kukufuru. Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake miezi arubaini na miwili.[#Dan 7:8,11,25; 11:36; Ufu 11:2; 12:6,14]

6Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni.

7Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa.[#Dan 7:21; Ufu 11:7]

8Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.[#Zab 69:28; Dan 12:1; Isa 53:7; Ufu 12:12; 3:5; 17:8]

9Mtu akiwa na sikio na asikie.

10Mtu akichukua mateka, atachukuliwa mateka. Mtu akiua kwa upanga, atauawa kwa upanga. Hapa ndipo penye subira na imani ya watakatifu.[#Yer 15:2; 43:11; Mt 26:52; Ufu 14:12]

Mnyama wa pili

11Kisha nikaona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka katika nchi; naye alikuwa na pembe mbili kama Mwana-kondoo, akanena kama joka.[#Ufu 16:13; Mt 7:15]

12Naye atumia uwezo wote wa mnyama yule wa kwanza mbele yake. Naye aifanya dunia na wote wakaao ndani yake wamsujudie mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona.

13Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu.[#Mt 24:24; 2 The 2:9,10; 1 Fal 18:24-39]

14Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi.[#Kum 13:2-4; Ufu 19:20]

15Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, ili ile sanamu ya mnyama iongee, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe.[#Dan 3:5,6]

16Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kulia, au katika vipaji vya nyuso zao;[#Ufu 19:20]

17tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa awe na chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya herufi za jina lake.

18Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.[#Ufu 17:9; 15:2; 1 Fal 10:14; Ezr 2:13]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya