Ufunuo 14

Ufunuo 14

Mwana-kondoo na wale watu 144,000

1Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu elfu mia moja na arubaini na nne pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao.[#Eze 9:4; Ufu 7:3; 3:12]

2Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao;[#Eze 1:24; 43:2; Ufu 1:15]

3na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; wala hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale elfu mia moja na arubaini na nne, walionunuliwa katika nchi.[#Zab 33:3; 40:3; 96:1; 98:1; 144:9; 149:1; Isa 42:10; Ufu 5:9]

4Hawa ndio wasiojitia unajisi na wanawake, kwa maana ni bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwana-kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-kondoo.[#2 Kor 11:2; Efe 5:27]

5Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa.[#Sef 3:13; Zab 32:2; Isa 53:9]

Ujumbe wa malaika watatu

6Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, akiwa na Injili ya milele, awahubirie hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa,[#Ufu 8:13]

7akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.[#Kut 20:11; Zab 146:6]

8Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.[#Isa 21:9; Yer 51:7,8; Ufu 18:2; Dan 4:30]

9Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake,[#Ufu 13:12-17; Mt 10:28]

10yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-kondoo.[#Isa 51:17; Mwa 19:24; Eze 38:22; Zab 75:8; Yer 25:15; Ufu 16:19]

11Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake.[#Isa 34:9,10; Ufu 19:3]

12Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.[#Isa 34:10; Ufu 13:10; 12:17]

13Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.[#Isa 57:2; Ebr 4:10; 1 Kor 15:58]

Kuvuna mavuno ya nchi

14Kisha nikaona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji la dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali.[#Dan 7:13; 10:16; Mt 13:39,41]

15Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa.[#Yoe 3:13]

16Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa.

17Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali.

18Na malaika mwingine akatoka katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sana.[#Yoe 3:13]

19Malaika yule akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu.[#Ufu 19:15]

20Shinikizo lile likakanyagwa nje ya mji, damu ikatoka katika shinikizo mpaka kwenye hatamu za farasi, kama mwendo wa maili mia mbili.[#Isa 63:3; Omb 1:15; Ufu 19:15; Yoe 3:13]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya