The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikaona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia.[#Law 26:21; Ufu 6:17; 12:1; 11:18]
2Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kandokando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi vya Mungu.[#Ufu 4:6; 13:15; 5:8]
3Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa.[#Kut 15:1,11; 34:10; Zab 111:2; 139:14; 145:17; Yer 10:6,7; Kum 32:4; Yos 14:7; Ufu 5:9]
4Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.[#Yer 10:7; Zab 86:9; Mal 1:11]
5Na baada ya hayo nikaona, na hekalu la hema ya ushuhuda mbinguni lilifunguliwa;[#Kut 38:21; 40:34; Ufu 11:19]
6na wale malaika saba, wenye mapigo saba, wakatoka katika hekalu, wamevikwa mavazi ya kitani safi, ya kung'aa, wamefungwa vifuani mwao mishipi ya dhahabu.[#Law 26:21; Eze 28:13]
7Na mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba vitasa saba vya dhahabu, vimejaa ghadhabu ya Mungu, aliye hai hata milele na milele.[#Ufu 4:6-8; 14:10]
8Hekalu likajazwa moshi uliotoka kwenye utukufu wa Mungu na uweza wake. Wala hapakuwa na mtu aliyeweza kuingia ndani ya hekalu, mpaka yatimizwe mapigo saba ya wale malaika saba.[#Kut 40:34; 1 Fal 8:10-11; 2 Nya 5:13-14; Isa 6:4; Eze 44:4]