The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa na ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake.[#2 Pet 2:4; Yud 1:6]
2Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;[#Mwa 3:1; Zek 3:1; Ufu 9:1; 12:9]
3akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia mhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe kwa muda mfupi.[#2 The 2:9,10]
4Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa mamlaka ya kutoa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala kuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.[#Dan 7:9,22,27; Lk 22:30; 1 Kor 6:2]
5Hao wafu waliobakia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.[#1 Kor 15:23; 1 The 4:16]
6Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu.[#Isa 61:6; Ufu 5:10]
7Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;
8naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.[#Eze 7:2; 38:2,9,15]
9Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala.[#Hab 1:6; 2 Fal 1:10; Eze 38:22; 39:6]
10Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.[#Mwa 19:24; Ufu 19:20]
11Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.[#Mt 25:31-46; Dan 2:35]
12Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, kulingana na matendo yao.[#Dan 7:10; Ufu 3:5; Flp 4:3; Rum 2:6]
13Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.[#Yn 5:28,29]
14Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.[#1 Kor 15:26,55]
15Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.[#Dan 12:1; Mt 25:41]