Ufunuo 22

Ufunuo 22

Mto wa maji ya uzima

1Kisha akanionesha mto wa maji ya uzima, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-kondoo,[#Eze 47:1; Zek 14:8]

2katikati ya njia yake kuu. Na upande huu na huu kando ya ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.[#Mwa 2:9; Eze 47:12; Ufu 21:21]

3Wala hapatakuwa na laana yoyote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumishi wake watamtumikia;[#Zek 14:11]

4nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao.[#Mt 5:8; Ufu 3:12]

5Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele.[#Isa 60:19; Dan 7:18,27; Ufu 21:25]

6Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi.[#Ufu 1:1; 1 Kor 14:32]

7Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.[#Ufu 3:11; 1:3]

Hitimisho na baraka

8Nami Yohana ndimi niliyeyasikia na kuyaona mambo hayo. Na hapo nilipoyasikia na kuyaona nilianguka, ili nisujudu mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionesha hayo.[#Ufu 19:10]

9Naye akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mtumishi mwenzako, na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu.

10Akaniambia, Usiyatie mhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.[#Ufu 10:4; 1:3; Dan 8:26; 12:4]

11Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.[#Dan 12:10]

12Tazama, naja upesi, na malipo yangu yako pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.[#Isa 40:10; 62:11; Zab 28:4; 62:12; Yer 17:10; Ufu 3:11; Rum 2:6]

13Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.[#Ufu 1:8,17; 2:8; Isa 44:6; 48:12; Ebr 13:8]

14Heri wazifuao nguo zao, ili wawe na haki ya kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.[#Mwa 2:9; 3:22; 49:11]

15Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.[#Ufu 21:8,27; 1 Kor 6:9,10]

16Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzawa wa Daudi, ile nyota yenye kung'aa ya asubuhi.[#Isa 11:1,2,10; 5:5; Isa 11:1,10; Lk 1:78; Ufu 1:1,2; 5:5]

17Roho na Bibi arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.[#Isa 55:1; Ufu 21:6; Zek 14:8; Rum 8:23; Yn 7:37]

18Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu yeyote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.[#Kum 4:2; 12:32; 29:20; Ufu 15:1,6]

19Na mtu yeyote akiondoa lolote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.[#Mwa 2:9; 3:22]

20Yeye ayashuhudiaye haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu.

21Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya