The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikaona Mwana-kondoo alipofungua mojawapo ya ile mihuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo![#Ufu 4:6; 5:1,2,6,8]
2Nikaona, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, huku akishinda tena apate kushinda.[#Zek 1:8; 6:3,6]
3Na alipoufungua mhuri wa pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema, Njoo!
4Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda aliruhusiwa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.[#Zek 1:8; 6:2]
5Na alipoufungua mhuri wa tatu, nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake.[#Zek 6:2,6]
6Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wanne, ikisema, Kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai.
7Na alipoufungua mhuri wa nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo!
8Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa wanyama wa nchi.[#Eze 5:12; 14:21; 29:5; 33:27; 34:28; Hos 13:14; Yer 15:3]
9Na alipoufungua mhuri wa tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao.[#Ufu 8:5; 14:18; 16:7]
10Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, na Mkweli, utakawia hadi lini kuhukumu na kuilipa damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi?[#Zek 1:12; Zab 79:10; Kum 32:43; Mwa 4:10; 2 Fal 9:7; Hos 4:1]
11Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wasubiri bado muda mchache, hadi itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu zao, watakaouawa kama wao walivyouawa.[#Ufu 3:4; 7:9; Mt 23:32]
12Nami nikaona, alipoufungua mhuri wa sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu,[#Ufu 11:13; 16:18; Isa 13:10; Yoe 2:10,31; 3:15; Mt 24:29; Mk 13:24-25; Lk 21:25; Eze 32:7,8]
13na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi.[#Isa 34:4; 13:10]
14Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake.[#Ufu 16:20]
15Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na muungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima,[#Isa 2:10,19,21; 24:21; 34:12; Yer 4:29; Zab 48:4; 2:2]
16wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na kwenye hasira ya Mwana-kondoo.[#Hos 10:8; Lk 23:30; Isa 6:1; Zab 47:8]
17Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kuistahimili?[#Yoe 2:11,31; Mal 3:2; Sef 1:14,18; Rum 2:5]