Ufunuo 7

Ufunuo 7

Waisraeli 144,000 waliotiwa mhuri

1Baada ya hayo nikaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za nchi, wakizizuia pepo nne za nchi, upepo usivume juu ya nchi, wala juu ya bahari, wala juu ya mti wowote.[#Yer 49:36; Dan 7:2; Zek 6:5; Eze 7:2; 37:9; Mt 24:31]

2Nikaona malaika mwingine, akipanda kutoka maawio ya jua, akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai; akawaita kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari,

3akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hadi tutakapokwisha kuwatia mhuri watumishi wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao.[#Eze 9:4,6]

4Nikasikia hesabu yao waliotiwa mhuri katika kila kabila la Waisraeli, watu elfu mia moja na arubaini na nne.[#Ufu 14:1,3]

5Wa kabila la Yuda elfu kumi na mbili waliotiwa mhuri.

Wa kabila la Reubeni elfu kumi na mbili.

Wa kabila la Gadi elfu kumi na mbili.

6Wa kabila la Asheri elfu kumi na mbili.

Wa kabila la Naftali elfu kumi na mbili.

Wa kabila la Manase elfu kumi na mbili.

7Wa kabila la Simeoni elfu kumi na mbili.

Wa kabila la Lawi elfu kumi na mbili.

Wa kabila la Isakari elfu kumi na mbili.

8Wa kabila la Zabuloni elfu kumi na mbili.

Wa kabila la Yusufu elfu kumi na mbili.

Wa kabila la Benyamini elfu kumi na mbili waliotiwa mhuri.

Umati wa watu kutoka kila taifa

9Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao;[#Ufu 6:11]

10wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-kondoo.[#Ufu 12:10]

11Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifudifudi mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu,[#Ufu 5:11; 11:16]

12wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina.

13Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Na wametoka wapi?

14Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-kondoo.[#Dan 12:1; Mt 24:21; Mk 13:19; Mwa 49:11; Ebr 9:14]

15Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao.[#Ufu 21:3,22]

16Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala joto iliyo yote.[#Isa 49:10]

17Kwa maana huyo Mwana-kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.[#Zab 23:1; Eze 34:23; Zab 23:2; Isa 49:10; 25:8; Ufu 5:6; Yer 2:13; 31:16]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya