The chat will start when you send the first message.
1Na Mwana-kondoo alipofungua mhuri wa saba, kukawa kimya mbinguni kwa muda wa kama nusu saa.[#Zek 2:13; Hab 2:20]
2Nami nikawaona wale malaika saba wasimamao mbele za Mungu, nao wakapewa baragumu saba.[#Mt 24:31]
3Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu, akiwa na chetezo cha dhahabu, akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi.[#Amo 9:1; Kut 30:1,3; Ufu 5:8]
4Na moshi wa ule uvumba ukapanda mbele za Mungu pamoja na maombi ya watakatifu, kutoka mkononi mwa malaika.[#Zab 141:2]
5Na huyo malaika akakitwaa kile chetezo, akakijaza moto wa madhabahu, akautupa juu ya nchi, kukawa radi na sauti na umeme na tetemeko la nchi.[#Law 16:12; Eze 10:2; Kut 19:16; Ufu 11:19; 16:18]
6Na wale malaika saba wenye baragumu saba wakajiweka tayari ili wazipige.
7Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyochangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea.[#Kut 9:23-25; Eze 38:22; Yoe 2:30]
8Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto, kikatupwa katika bahari; theluthi ya bahari ikawa damu.[#Yer 51:25; Kut 7:20,21]
9Wakafa theluthi ya viumbe vilivyomo baharini, vyenye uhai; theluthi ya meli zikaharibiwa.
10Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya theluthi ya mito, na juu ya chemchemi za maji.[#Isa 14:12; Dan 8:10]
11Na jina lake ile nyota yaitwa Pakanga; theluthi ya maji ikawa pakanga, na wanadamu wengi wakafa kwa maji hayo, kwa kuwa yalifanywa kuwa machungu.[#Yer 9:14]
12Malaika wa nne akapiga baragumu, theluthi ya jua ikapigwa, na theluthi ya mwezi, na theluthi ya nyota, ili kwamba ile theluthi itiwe giza, mchana usiangaze theluthi yake, na usiku vivyo hivyo.[#Isa 13:10; Eze 32:7; Yoe 2:10,31; 3:15; Ufu 6:12; Kut 10:21]
13Kisha nikaona, nikasikia tai mmoja akiruka katikati ya mbingu, akisema kwa sauti kuu, Ole, ole, ole wao wakaao juu ya nchi! Kwa sababu ya sauti za baragumu ziliobakia za malaika watatu, walio tayari kupiga.[#Ufu 9:12; 11:14]