The chat will start when you send the first message.
1Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.[#Mdo 22:3]
2Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa.
3Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.[#Rum 9:31,32]
4Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki.[#Mt 5:17; Yn 3:18; Ebr 8:13]
5Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo.[#Law 18:5; Gal 3:12]
6Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, kumleta Kristo chini),[#Kum 30:12-14]
7au, Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.)
8Lakini yanenaje? Lile neno liko karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.[#Kum 30:14]
9Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.[#2 Kor 4:5]
10Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.
11Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.[#Isa 28:16]
12Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Mgiriki; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye ukarimu mwingi kwa wote wamwitao;[#Mdo 10:34; 15:9; #10:12 Au ‘mwenye utajiri’.]
13kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.[#Yoe 2:32]
14Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?
15Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema![#Isa 52:7]
16Lakini si wote walioitii ile Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu?[#Isa 43:1]
17Basi imani, hutokana na kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.[#Yn 17:20]
18Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia,[#Zab 19:4]
Sauti yao imeenea duniani kote,
Na maneno yao hadi katika miisho ya ulimwengu.
19Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena,[#Kum 32:21]
Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa,
Kwa taifa lisilo na fahamu nitawakasirisha.
20Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema,[#Isa 65:1]
Nilipatikana nao wasionitafuta,
Nilidhihirika kwao wasioniulizia.
21Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa niliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.[#Isa 65:2]