Warumi 13

Warumi 13

Kutii mamlaka

1Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.[#Tit 3:1; Yn 19:11; Mit 8:15]

2Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.

3Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;[#1 Pet 2:13,14; 3:13]

4kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.[#Zab 82:6; Rum 12:19]

5Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.

6Kwa sababu hiyo tena mnalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo.[#Mt 22:21; Mk 12:17; Lk 20:25]

7Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima.[#Mt 22:21]

Upendo

8Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria.[#Gal 5:14; 1 Tim 1:5]

9Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yoyote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako.[#Kut 20:13-15,17; Kum 5:17-19,21; Law 19:18]

10Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.[#1 Kor 13:4; Mt 22:40]

Ombi la dharura

11Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu uko karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini[#Efe 5:14; 1 The 5:6,7]

12Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru.[#1 Yoh 2:8; Efe 5:11; 2 Tim 1:10]

13Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.[#Lk 21:34; Efe 5:18]

14Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.[#Gal 3:27]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya