The chat will start when you send the first message.
1Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe.
2Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake, apate wema, akajengwe.[#1 Kor 9:19; 10:24,33]
3Kwa maana Kristo naye hakujipendeza mwenyewe; bali kama ilivyoandikwa, Matusi yao waliokutusi wewe yalinipata mimi.[#Zab 69:9]
4Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya Maandiko tupate kuwa na tumaini.[#Rum 4:23,24; 1 Kor 10:11]
5Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunuia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu;[#Flp 3:16]
6ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
7Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe.
8Kwa maana nasema, ya kwamba Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu;[#Mt 15:24; Mdo 3:25]
9tena ili Mataifa wamtukuze Mungu kwa ajili ya rehema zake; kama ilivyoandikwa,[#2 Sam 22:50; Zab 18:49; Rum 11:30]
Kwa hiyo nitakushukuru kati ya Mataifa,
Nami nitaliimbia jina lako.
10Na tena anena,[#Kum 32:43]
Furahini, Mataifa, pamoja na watu wake.
11Na tena,[#Zab 117:1]
Enyi Mataifa yote, msifuni Bwana;
Enyi watu wote, mhimidini.
12Na tena Isaya anena,[#Isa 11:10; Ufu 5:5]
Litakuwako shina la Yese,
Naye aondokeaye kuwatawala Mataifa;
Ndiye Mataifa watakayemtumaini.
13Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu.
14Ndugu zangu, mimi mwenyewe nina hakika juu yenu, kuwa ninyi mmejaa wema, na mmejazwa ujuzi wote, tena mnaweza kuonyana.
15Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu,[#Rum 1:5; 12:3]
16ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu.[#Rum 11:13; Flp 2:17]
17Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu.
18Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo,[#2 Kor 3:5]
19kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kandokando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu;[#Mk 16:17]
20kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine;[#2 Kor 10:15,16]
21bali kama ilivyoandikwa,[#Isa 52:15]
Wale wasiowahi kuhubiriwa habari zake wataona,
Na wale wasiowahi kusikia habari zake watafahamu.
22Ndiyo sababu nilizuiwa mara nyingi nisije kwenu.[#Rum 1:10-13]
23Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena kwa miaka mingi nimekuwa nikitamani kuja kwenu;
24wakati wowote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana natarajia kuwaona ninyi nikiwa katika safari, na kusafirishwa nanyi, baada ya kukaa kwenu kwa muda.[#1 Kor 16:6]
25Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumia watakatifu;[#1 Kor 16:1-4; #Mdo 19:21; 20:22]
26maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kutoa mchango kwa ajili ya watakatifu walio maskini huko Yerusalemu.[#1 Kor 16:1; 2 Kor 8:1; 9:2,12]
27Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumia kwa mambo yao ya mwili.[#1 Kor 9:11; Rum 9:4]
28Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia mhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania.
29Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo.[#Rum 1:11]
30Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu;[#2 Kor 1:11; Flp 1:27; Kol 4:3; 2 The 3:1]
31kwamba niokolewe kutoka kwa wale wasioamini katika Yudea, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu;
32nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi.
33Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amina.